Mawaziri watatu nchini Tunisia wamejitoa kwenye serikali ya umoja wa kitaifa siku moja tu baada ya kutangazwa.
Viongozi hao watatu ni kutoka General Union of Tunisian Workers (UGTT), chama kilichochangia katika maandamano kwa kiasi kikubwa na kusababisha kukimbia kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo.
Waziri mkuu Mohammed Ghannouchi aliwakasarisha waandamanaji wengi alipowabakiza mawaziri wengi kutoka chama tawala kwenye serikali hiyo.
Maandamano mapya yameripotiwa kuibuka nchini kote.
Bw Ghannouchi alitarajia kutuliza maandamano hayo siku ya Jumatatu kwa kutangaza serikali umoja wa kitaifa- iliyojumuisha wapinzani lakini pia kuwabakiza wanachama wa chama tawala RCD katika nafasi muhimu za uwaziri.
Lakini baadhi ya waandamanaji wametangaza kuwa uongozi mpya umewasaliti.
Na sasa naibu waziri wa uchukuzi, Anouar Ben Gueddour, alisema yeye na mawaziri wengine wawili, Abdeljelil Bedoui na Houssine Dimassi, wanaondoka.
Wote watatu ni wanachama wa UGTT.
Sababu za mawaziri hao kubadili msimamo wao haujaweza kujulikana.
Hata hivyo, ripoti moja ilisema UGTT iliamua kutoitambua serikali mpya.