MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi `Sugu’ amewaonya askari Mgambo wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wanaotumia mabavu kunyang’anya bidhaa za wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga kwa kisingizio cha kuzifikisha katika Ofisi za Jiji, na
badala yake hutumia nafasi zao kujinufaisha binafsi.

Mbilinyi aliyasema hayo hivi karibuni na kubainisha kuwa, ameshazungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri, Juma Idd na kukanusha kuwaagiza Mgambo kwenda kuwakamata wafanyabiashara hao katika kipindi cha hivi karibuni.
 Mbunge huyo alisema kitendo cha Mkurugenzi kukataa kinaonesha kuwa Mgambo wamekuwa wakijiamulia kuingia mitaani na kunyang’anya bidhaa za wafanyabiashara wanaodaiwa kufanyia shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi na kusisitiza kuanzia sasa hatayavumiliwa matukio ya aina hiyo.

Alishangazwa kuona kuwa bidhaa nyingi zinazokamatwa ni zile za vyakula ambazo licha ya
kukamatwa na kuchanganywa kisha kubebwa kusikofahamika, Mgambo hao kamwe hawachanganyi vyakula vya nafaka visivyo rahisi kuchambuliwa.

Aliwataka Mgambo hao kutambua kuwa biashara ndogondogo ni mbadala wa shughuli haramu za upigaji nondo zilizokuwa zikifanywa na vijana katika maeneo mbalimbali jijini hapa hivyo wanapaswa kuona hatua ya vijana hao kuanza kujishughulisha inastahili pongezi.

“Tunapaswa kuwapongeza vijana kwa sababu kwa sasa wameacha nondo na kuzigeukia biashara. Hii ni faida kubwa kwetu kwakuwa kwa sasa tunaishi kwa amani hata Jeshi la Polisi chini ya RPC Nyombi limekiri kuwa vitendo vya upigaji nondo vimepungua. Sasa wenzetu wanataka kuwarejesha vijana huko, hatukubali,” alisema Mbilinyi.

Alisema wazo la Halmashauri kuwataka wafanyabiashara kufanyia shughuli zao katika maeneo yaliyotengwa rasmi si baya, lakini akashauri si vyema kuanza kuwasumbua kabla ya kuoneshwa mahali wanapostahili kuendeshea shughuli zao.