Magoli kutoka kwa winga Mrisho Ngassa, mshambuliaji John Bocco na jingine lililoonekana la kujifunga kutoka kwa kipa Juma Kaseja, yaliwashushia mabingwa Simba kipigo chao cha tatu cha ligi msimu huu wakati walipolala 3-2 dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba, ambao katika mzunguko wa kwanza wa ligi walilala isivyotarajiwa kwa Polisi Dodoma kabla ya kupigwa 1-0 na mahasimu yao Yanga, walianza mechi ya jana kwa kasi na walihitaji dakika 8 tu kupata goli la kwanza kupitia kwa mshambuliaji wa timu ya taifa, Rashid Gumbo aliyemzidi ujanja beki Aggrey Morris.