Mfungwa wa kwanza katika jela ya Guantanamo kushtakiwa kwenye mahakama ya kiraia, Ahmed Ghailani kutoka Tanzania amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Hukumu hiyo ilitolewa na mahakama ya jimbo la Manhattan.
Jopo la majaji hata hivyo limempata na hatia ya kufanya njama ya kuharibu majengo ya serikali.

Upande wa mashtaka ulijaribu kumshawishi jaji kwamba Ghailani alipaswa kuonewa huruma kwa sababu hakujua kuhusu njama hiyo.
Vile vile walisema kuwa Ghailani aliteswa na CIA baada ya kukamatwa.
Hata hivyo waendesha mashtaka walitaka apewe kifungo cha maisha gerezani huku wakisisitiza kuwa alijua kuhusu njama hiyo.
Akijiandaa kutoa hukumu yake, Lewis A. Kaplan alisema ilikuwa siku ya haki kwa jamii za watu 224 waliofariki kwenye mashambulizi ya bomu ya mwaka wa 1998 pamoja na wale wote waliojeruhiwa.
Kaplan alisema aliridhishwa na ushahidi aliopata kwamba Ghailani alijua kwamba watu wangekufa kutokana na vitendo vyake.
Ghailani alikamatwa nchini Pakistan mwaka 2004.
Alipelekwa kwenye kambi ya siri inayosimamiwa na shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, kabla ya kupelekwa Guantanamo Bay, Cuba, mwaka 2006.
Baadaye alihamishwa hadi New York alikoshtakiwa.