Kama ukibahatika kufika sehemu za Yombo Kilakala maarufu kama Chedi au Sharp Corner na kumuulizia huyu fundi simu MUSA NJECHELE nafikiri hata mtoto mdogo atakufikisha mahala alipo fundi huyu.Musa ana ulemavu wa macho, lakini ameweza kufungua kibanda cha kutoa huduma za simu ikiwa ni pamoja na kutengeneza simu.
 Kwa kifupi, ni fundi mahiri wa simu. Na hilo unaweza kulithibitisha kama utafika katika ofisi yake aliyoibatiza jina la Muzunje Inclusive Service, iko eneo la Yombo Kilakala iliyopo Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Anafafanua kuwa jina hilo la Muzunje linatokana na herufi za kwanza za majina yake yaani Musa Zuberi Njechele. Hapo utakutana na watu wanaopishana kuingia katika ofisi yake kwa lengo la kujipatia ama huduma ya kupiga simu, kununua vocha au kutengenezewa simu.
Mwenyewe, akizungumza Jumapili hii anasema kwamba, miujiza yote hiyo imekuja ndani ya kipindi kifupi cha miaka saba tu, kwani alianza ufundi wa simu mwaka 2003, baada ya kufanikiwa kumiliki kwa mara ya kwanza simu ya mkononi.

Anasema kwamba, kutokana na ugumu wa biashara za vifaa vya simu aliamua pia kufanya biashara ndogo ndogo na kuajiri binti wa kuuza vocha za simu ambaye pia alimsaidia kuangalia watu wakorofi wasiibe simu kwa kuwa yeye haoni.

Njechele ambaye kitaaluma ni mwalimu, anasema alipoanza biashara ya simu mwaka 2003 alikuwa anafanyia kazi katika mazingira duni kwenye kibanda cha mbao, baada ya miezi saba akahamia kwenye kontena la mabati lenye ukubwa wa futi nane kwa saba.

Agosti mwaka jana aliweza kupangisha fremu iliyojengwa kwa tofali na bati sehemu anayofanyia biashara zake hadi leo. Anasema kazi hiyo imemuwezesha kuongeza pato la familia yake pamoja na kutoa nafasi za ajira isiyo rasmi kwa vijana watano kwa nyakati tofauti.

Awali aliajiri msichana na huduma ya kutengeneza simu ilipopanuka aliamua kuajiri vijana wawili. Kwa kutambua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, aliamua kuwafundisha wadogo zake shughuli za ujasiriamali pamoja na kutengeneza simu za mkononi.

Mjasiriamali huyo anasema kuwa, alianza kujishughulisha na biashara ndogo ndogo angali kijana mdogo wakati akisoma Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Ilala jijini Dar es Salaam na wakati wa likizo alipokuwa akisoma sekondari.

Anaikumbuka historia yake kwa kusema kuwa, alizaliwa Mei mwaka 1971 jijini Dar es Salaam, akiwa hana tatizo la kuona. Hata hivyo balaa lilimfika akiwa na umri wa miaka minane, baada ya kupoteza kabisa uwezo wa kuona na anasema alielezwa hali hiyo ilitokana na madhara aliyopata katika mishipa ya macho baada ya kuugua surua.

Mwaka 1982 alianza darasa la kwanza katika Shule ya Uhuru Mchanganyiko iliyopo Dar es Salaam na kuhitimu elimu ya msingi mwaka 1988. Kwa kuwa alikuwa anaishi na bibi yake ambaye hakuwa na uwezo wa kumnunulia mahitaji muhimu ya shule, kila alipofunga shule alifanya biashara ndogo ndogo ili kupata fedha za kujikimu na kununua vifaa vya shule.

“Kutokana na hali yangu ya ulemavu nililazimika kusoma shule ya bweni kuanzia elimu ya msingi. Hivyo nilipokuwa msingi niliuza matunda na maji na wakati nikiwa sekondari nilishona na kupiga rangi viatu,” anaeleza.

Kwa kuwa alifaulu vizuri mtihani wa Taifa ya kuhitimu elimu ya msingi alipangiwa kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Ufundi Shinyanga. Anasema ingawa alipenda masomo ya Sayansi na Teknolojia, alipokuwa sekondari alisoma masomo ya sanaa hivyo kukosa fursa ya kujifunza kemia, fizikia, biolojia na hisabati.

“Mwanzoni mwa miaka ya 1990 shule nyingi za sekondari hazikuwa na nyenzo za kufundisha hisabati na masomo ya sayansi kwa wasioona,” alisema. Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari aliamua kutumia kipaji chake katika masuala ya ujasiriamali na kusafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Anasema mwaka 1993 alifanya utafiti na kubaini kuwa Tanzania Bara kuna soko kubwa la biashara ya nguo kutoka Zanzibar na wakati huo huo Zanzibar kulikuwa na soko la vyombo vya udongo kutoka Bara.

“Sikupenda kupoteza wakati, nilinunua vyombo vya udongo na kwenda kuviuza Zanzibar na wakati wa kurudi nilileta nguo na kuziuza Dar es Salaam,” anaeleza. Mwaka 1994 alipata nafasi ya kusomea ualimu kati Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Dodoma.

Anakumbuka kuwa, akiwa katika chuo hicho alisikia tangazo la kozi ya kushona viatu na aliichangamkia, ikiwa ni sehemu ya masomo ya ziada. “Kwa kuwa nilikuwa na uzoefu wa kushona viatu niliamua kujiunga….nakumbuka tulijitokeza wanafunzi wanane.

Walipata mashaka kama ningeweza kutokana na hali yangu ya ulemavu,” anaeleza. Hata hivyo aliwaondoa walimu wake wasiwasi kwa kuwa baada ya kupatiwa mtihani wa majaribio alifanya vizuri kuliko wanafunzi wengine.

Njechele alihitimu kozi ya ualimu mwaka 1996 na mwaka 1997 alimua kujiajiri mwenyewe kama fundi viatu, ili kuepuka adha inayowakabili vijana wanaokaa vijiweni kutokana na ukosefu wa ajira.

Pia aliamua kufungua darasa la masomo ya ziada kwa wanafunzi wa shule ya msingi maarufu kama twisheni ili kuimarisha kipato chake na kutumia taaluma yake ya ualimu. “Kazi ya ufundi viatu ndio iliniweka mjini na kuniwezesha kuoa mke wangu wa kwanza,” anasema Njechele ambaye alitengana na mke wake wa kwanza na sasa ana `mama’ mwingine.

Mwaka 1998 alisikia tangazo la kazi ya ualimu mkoani Mbeya na kutuma maombi ili kubahatisha bahati yake. “Kweli nilifanikiwa na Januari mosi mwaka 1999 nilianza kazi ya ualimu katika Shule ya Msingi Katumbu Mbili.

Anasema mwaka 2002 aliomba uhamisho kuja Dar es Salaam ili aweze kukaa karibu na familia yake na akapangiwa kufundisha Shule ya Msingi Sandali, iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam. “Nilipokuja Dar ndipo nikabahatika kuona (kumiliki) simu ya mkononi Siemens C35 ambayo unaweza kupiga ukiwa popote na kuzunguka nayo kokote utakapo…nilifurahi na kustaajabu sana,” anaeleza.

Mwaka 2003 alifanikiwa kumiliki simu aina ya Sony Ericsson 1018. Hata hivyo Njechele hana uwezo wa kuona hata kidogo. Anaposema aliona anamaanisha kuwa aliishika na kuipapasa, akasikia mlio na akazungumza na simu kwa hiyo akiwa anahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Anafahamisha kuwa alifurahi sana na kuweka mikakati ya kumiliki simu. Akifanikisha ndoto yake mwaka 2003 baada ya kufanikiwa kununua simu aina ya Sony Ericsson 1018. Kwa kuwa alikuwa na shauku ya kuona muundo wa simu, alidhamiria kuwa fundi simu jambo ambalo lilimpa msukumo wa kuifungua simu yake na kudadisi ilivyotengenezwa.

“Mwaka 2003 ndipo nilianza kazi ya kutengeneza simu...kwa kuwa sikuwa na uwezo wa kuona niliwasiliana na mafundi wengine na kunipa maelezo ya vifaa vilivyo ndani ya siku,” anafahamisha.

Anasema ilikuwa vigumu watu kumuamini hivyo alianza kwa kuuza vocha za simu, kurekebisha tarehe na saa na kuweka nyimbo kwenye simu.

“Biashara ni uthubutu...ingawa sikuwa na uwezo wa kuona niliweza kurekebisha simu mpya kwa kuchagua lugha, mfumo wa kutuma ujumbe mfupi, tarehe na muda jambo ambalo liliwezesha watu kujenga imani na mimi,” anaeleza.

Baada ya muda mfupi aliweza kutengeneza simu zilizoharibika na hivi sasa ameweza kupanua huduma hiyo na kuajiri vijana wawili. Kama ilivyo kwa mafundi wengine, anakabiliwa pia na changamoto hasa pale anaposhindwa kutengeneza simu ambayo imeharibika kabisa.

“Ninapopokea simu ya mteja anakuwa na matumaini makubwa kuwa inapona, lakini wakati mwingine unakuta imeharibika sehemu kubwa ama gharama za kuitengeneza ni sawa na kununua simu mpya, ukimjulisha mteja ukweli anachukia na kukudharau,” anaeleza.

Pia anasema kadiri simu zinavyosonga mbele ndivyo teknolojia ya mawasiliano ya simu inavyokuwa na baadhi ya simu zinatumia malighafi, laini hivyo kuwa vigumu kusomwa na wasioona.

Hata hivyo kazi hiyo ni ya ziada. Njechele bado ni Mwalimu katika Shule ya Msingi Sandali na anafundisha masomo ya Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Anasema ingawa wanafunzi hawana kompyuta za kujifunza kwa vitendo, Njechele anasema wana uwezo wa kufuatilia vyema masomo ya nadharia.

Yeye ana uwezo wa kutumia kompyuta kwa kutumia programu maalumu zinazowasaidia wasioona kama vile programu ya Dolphin, Narrator na Screen wonder. Anasema ndoto zake za baadaye ni kumiliki duka kubwa la simu pamoja na kufundisha vijana jinsi ya kutumia teknolojia ya kisasa.

Hata hivyo mtaji ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokwamisha ndoto yake. Anaomba wenye uwezo wa kumsaidia au kumwelekeza jinsi ya kuboresha biashara yake. Anapatikana kwa simu namba 0715 966 224.

Anapendelea michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu na michezo yote ya wasioona, kusikiliza redio, kuchanganyika na watu na kujifunza mambo mbalimbali hasa ufundi.

Anaomba jamii isiwatenge watu wenye ulemavu, bali iwasaidie wenye uthubutu wa kujituma na kuhamasisha wale wasiokuwa na uthubutu ili kuondoa dhana kuwa wenye ulemavu hawawezi kufanyakazi na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Huyo ndiye Musa Zuberi Njechele, mlemavu asiyeona aliyethubutu kufanya mambo makubwa licha ya hali aliyonayo. Kwa hakika, ni mfano wa kuigwa na nyota wa kweli katika jamii hii iliyozungukwa na vijana wengi wanaobweteka na kushinda vijiweni kwa kisingizio cha kukosa ajira.