Prof. Abdallah Safari (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Alhamisi, na akatangaza kujivua uanachama wa Chama Cha Wananchi (CUF).Akizungumza Dar es Salaam jana huku akitoa siri zilizofanya ajivue uanachama huo, alisema kwa sasa chama hicho hakina mwelekeo wa kuwa cha kitaifa kutokana na kuegemea zaidi Zanzibar hali iliyowafanya wanachama wake wengi wa Tanzania Bara kukiona kama chama cha Wapemba. Pia alikituhumu chama hicho kwa kukosa mfumo wa kidemokrasia katika uongozi na badala yake kuwa na mfumo ulioegemea zaidi katika usultani na ufalme kwa madai kuwa wanachama wengi wanashindwa kuwania nafasi za ngazi za juu za uongozi.

“Nachukua uamuzi huu kwa uchungu sana, nimeutafakari kwa takribani miaka miwili sasa na nimeamua kujitoa kwenye chama hiki cha CUF ingawa uamuzi huu haumaanishi kuwa ndio naachana na siasa, la hasha,” alisema Prof. Safari.

Alisema, alijiunga na chama hicho mwaka 2005 baada ya kurejea nchini akiwa na mkewe wakitokea Uingereza na walivutiwa na CUF kutokana na jina lake alilosema liliwagusa moja kwa moja wananchi, lakini pia kaulimbiu yake iliyosema haki sawa kwa wote.

Alisema pia wakati huo chama hicho kilikuwa na wanachama wenye majina makubwa kama vile James Mapalala, Msomi Mmwageni, Fatma Magimbi, Wilfred Lwakatare, Akwekumbe Christopher, Ramadhan Mzee na Tamwe Hizza ambao wote kwa sasa wameondoka.

“Sote tunafahamu kuwa chama ili kiwe kizuri, inategemea na safu ya watu waliopo ndani ya chama hicho. Kwa sasa CUF haina watu kama zamani na wala hakuna jitihada za kuwatafuta, yaani kimeshindwa kuwavuta hata wasomi,” alisema.

Kwa mujibu wa Prof. Safari, wakati akijiunga na chama hicho, kilikuwa na nguvu kubwa kiasi cha kuwavuta watu wengi kila kinapofanya mikutano yake, lakini kwa sasa chama hicho hata Mwenyekiti wake Profesa Lipumba akiitisha mkutano wa hadhara, ni watu wachache tu watakaojitokeza.

Alisema hali hiyo inatokana na wananchi kukiona chama hicho cha upande mmoja wa Zanzibar kwa kuwa hata jitihada za viongozi wake zimeegemea zaidi kupata uongozi visiwani humo.

Kuhusu ukosefu wa demokrasia, alitolea mfano uchaguzi wa viongozi wa ndani ya chama hicho uliofanyika mwaka juzi ambapo yeye aliwania nafasi ya uenyekiti iliyokuwa ikishikiliwa na Prof. Lipumba.

“Nilipoamua kuwania nafasi ya uenyekiti, ilikuwa kama vile nimetangaza vita na Lipumba, nia yangu ilikuwa ni kurejesha nguvu ya kitaifa ndani ya chama hiki, lakini kwa hali ilivyokuwa ni kama vile mtu anapotaka kuwania nafasi za juu za uongozi anatangaza uhasama,” alisema.

Alisisitiza madai yake, safari hii kwa kutaja vyeo kwamba katika chama hicho nafasi ya uenyekiti na ukatibu mkuu iko katika mfumo wa kisultani au kifalme na kama ina wateule wawili, Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa Lipumba na mtu yeyote akitaka kuwania nafasi hizo hujikuta katika wakati mgumu.

Akisimulia yaliyompata alipoamua kuwania nafasi hiyo ya uenyekiti, alidai alihojiwa na Maalim Seif akitakiwa kueleza mchango wake ndani ya chama hicho, hali ambayo ilimsikitisha kwa kuwa alipoteza kazi yake katika Chuo cha Diplomasia kwa sababu ya chama hicho.

Mbali na usultani huo, sababu nyingine aliyodai Prof. Safari kuwa imemfanya ajitoe katika chama hicho ni kutofautiana kimsimamo na uongozi wa chama hicho.

“Wakati wa uchaguzi nilishauri CUF tusishiriki kwenye uchaguzi iwapo hakutakuwa na tume huru ya uchaguzi, lakini wenzangu walinipinga na kudai hawawezi kumuachia nguruwe shamba la mihogo,” Hata hivyo Profesa Safari hakusema baada ya kujitoa kwenye chama hicho ana mpango wa kuhamia chama gani cha siasa na alisisitiza hatojiunga na chama chochote hadi pale atakapopata chenye mwelekeo wa kitaifa, kinachochukia ubinafsi, dhuluma na ubaguzi wa aina yoyote.

Tofauti na baadhi ya wanachama wengine wa chama hicho waliojiengua, Prof. Safari aliweka wazi kuwa hana mpango wa kujiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM) wala Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Alisema uamuzi huo umetokana na alichodai kuwa ni uhalisia wa vyama hivyo hasimu katika siasa za Tanzania Bara kuwa na matatizo.

Hata hivyo hakuficha kuwa amepata mialiko ya kuwa mwenyekiti kutoka kwa vyama vitatu vya siasa ambavyo hakuvitaja jambo linaloonesha alishaanza kuelezea mwelekeo wake ndani ya CUF, kabla hata ya kutangaza kujivua uanachama.

Katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya uenyekiti katika chama hicho, Profesa Safari alijitosa na kuzua mtafaruku ndani ya chama hicho ambapo hata hivyo Profesa Lipumba alimbwaga vibaya katika uchaguzi huo.