Huku hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) iliyoipa ushindi kampuni ya Dowans Tanzania Limited dhidi ya Shirika la Umeme nchi (Tanesco) kuwa ilipwe fidia ya Sh. bilioni 94 ikisubiriwa kusajiliwa rasmi Mahakama Kuu, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amekuwa mbogo upya.
Safari hii Sitta, ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa serikali ya awamu ya nne kutoa maoni makali juu ya hukumu hiyo inayotaka Tanesco wailipe Dowans fidia ya Sh. bilioni 94 kwa kuvunja mkataba wa kufua umeme wa dharura mwaka 2008, amesema kamwe hatafungwa mdomo wala kuwasaliti Watanzania kubadili msimamo wake wa kupinga uamuzi wa serikali wa kukubali Tanesco iilipe Dowans fidia hiyo.
Waziri Sitta alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, ikiwa ni siku moja tu baada ya gazeti hili kuandika habari kuwa hukumu ya ICC ya Dowans dhidi ya Tanesco ilikuwa imekwisha kuwasilishwa Mahakama Kuu kwa usajili ikiwa ni hatua muhimu kwa ajili ya malipo hayo kufanyika.
Sitta alisema hatafunga mdomo si Dowans tu, bali pia katika kujadili mambo yote yanayohusu nchi na wananchi.
Waziri Sitta alisema ana uhakika wa asilimia zote kwamba, hawezi kufungwa mdomo kujadili mambo hayo kwa vile siku zote yupo kwa ajili ya wananchi na nchi na si vinginevyo.
Alisema uthibitisho wa hilo unatokana na ukweli kwamba, tangu atangaze msimamo wake wa kupinga malipo hayo kwa Dowans, hajaulizwa wala kutishwa popote wala na mtu yoyote zaidi ya taarifa za kupikwa, ambazo hata hivyo, hakueleza ni zipi.