Kamanda wa jeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameshutumiwa kwa kuongoza ubakaji wa wanawake takriban 50 uliofanyika hivi karibuni.
Mmoja wa waliobakwa, pamoja na vyanzo vilivyonukuliwa katika ripoti ya umoja wa mataifa, wote wanamshutumu Lt Col Kibibi Mutware kwa kuhusika na ubakaji huo uliofanyika mwaka mpya mjini Fizi.
Kumekuwa na ripoti nyingi za ubakaji huko Congo lakini tukio hili linaaminiwa kuwa la kwanza kwa idadi kubwa ya wanawake kubakwa likihusishwa jeshi.
Lt Col Kibibi amekana tuhuma hizo.
Alisema wanajeshi waliovamia eneo hilo walikiuka amri.
Kutokana na ugomvi baina ya wanaume wawili waliokuwa wakimgombea mwanamke, ghasia hizo zikazidi ambapo jeshi la serikali likaanza kuwaadhibu watu wa Fizi.

'Aibu'

Dr Faise Chacha, mkuu wa hospitali ya Fizi ameeleza, " Askari mmoja aliuawa hapa karibu kabisa na hospitali hii."
"Hiyo ilisababisha wasiwasi na wagonjwa wetu wote wakakimbia. Tulirudi siku ya pili asubuhi na tukaanza kuwapokea watu waliokuwa wamepigwa kisu na wengine- wanawake- waliobakwa."
Dr Chacha na shirika la kitabibu la kutoa msaada Medecins Sans Frontieres wamewatibu waathirika 51 waliobakwa mpaka sasa.
Kama ilivyo kwa matukio ya awali huko Congo, wengi wanatarajiwa kuficha yaliyowasibu kuepuka kuachwa na waume na familia zao.
Wawili miongoni mwa wanawake hao walikubali kuzungumza na BBC ilimradi tu wasitajwe majina yao.
Mmoja aliiambia BBC, " Nilibakwa mbele ya watoto wangu wanne."
"Ninaona aibu, ninaona aibu sana. Nikikutana na watu wawili au watatu ambao wanajadili jambo, naanza kuhisi tu kuwa wananizungumzia mimi, hata kama si kuhusu mie."
Mwanamke huyo mwengine alifanikiwa kumtambua aliyembaka.
"Ilikuwa jioni na walionibaka walikuwa wanajeshi," alisema kwa sauti ndogo, mwili wake ukiwa umefunikwa na khanga yenye rangi za kuvutia.
" Walikuwa wanne- Kibibi na walinzi wake. Wameiba vitu vyetu vyote pamoja na pesa."