Takriban watu wawili wameuawa katika mapigano baina ya watu wanaowaunga mkono wapinzani wa nafasi ya urais huko Ivory Coast.
Miili ya raia wawili iliyokuwa na majeraha ya risasi walionekana eneo la Abobo, Abidjan, ngome ya Alassane Ouattara.
Bw Ouattara anatambulika kimataifa ndiye aliyeshinda katika uchaguzi wa mwezi Novemba, lakini mpinzani wake, Laurent Gbagbo, amekataa kukubaliana na hali hiyo.
Mamia ya polisi waliripotiwa kufanya doria eneo hilo la Abobo siku ya Jumanne.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban watu 200 wameuawa katika mapigano ya hapa na pale tangu uchaguzi.
Uchaguzi huo wa Rais ulitakiwa kuiunganisha Ivory Coast, iliyogawanyika baina ya kaskazini na kusini tangu ghasia za mwaka 2002.
Bw Ouattara amezuiwa kwa wiki kadhaa katika hoteli huko Abidjan, mji mkuu wa Ivory Coast, akilindwa na majeshi ya kutunza amani ya umoja wa mataifa na majeshi mapya ya waliokuwa waasi wanaodhibiti upande wa kaskazini mwa nchi hiyo.