SERIKALI imebaini kuwa baadhi ya watumishi wa huduma ya afya wa kada ya wasaidizi wa daktari, wanaongoza kwa utoaji mimba kiholela katika hospitali za watu binafsi, huku za mashirika ya dini zikitumia vibaya vibali vya kununua dawa za Serikali. Alisema tatizo lingine lililobainika ni baadhi ya hospitali na vituo vya afya vya mashirika ya dini kupewa kibali cha kununua dawa serikalini na kuziuza katika hospitali za watu binafsi kwa bei kubwa.

“Kutokana na vituo vya dini kutoa huduma bila faida, zinapewa vibali vya kununua dawa za Serikali ili kuzitoa kwa wananchi kwa bei nafuu, lakini wamekuwa wanavitumia vibaya kwa kuuza dawa hizo kwa hospitali binafsi, hivyo kuwauzia wananchi mara mbili ya bei inayouzwa na Serikali,” alisema.

Alisema baadhi ya dawa walizozikuta kwenye hopitali hizo ni za malaria; za Aluu, antibiotic
na pia vifaa vilivyoibwa katika hospitali za Serikali kama vile mabenchi.

Dk. Sawa aliongeza: “Kusema ukweli kuna matatizo mengi ya utoaji huduma za afya, na hii inaonesha maisha ya wananchi hayako salama, kwani vituo vingi ni bubu, hakuna watumishi wenye taaluma, vifaa vya kutolea huduma ni duni kwa baadhi ya hospitali, kufanya vipimo kwa ubabaishaji na huduma inatolewa katika mazingira hatarishi.”

Akitolea mfano wa Hospitali ya Mawenzi, Moshi, alisema chumba cha upasuaji mdogo kimetakiwa kufanyiwa marekebisho na cha upasuaji mkubwa kimefungwa na tatizo hilo pia limejitokeza katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambayo chumba cha kuzalia na upasuaji havikufaa na pia chumba cha X-Ray kilikuwa kinatoa mionzi ambayo inaathiri watu.

“Tumekwenda kufanya ukaguzi katika Hospitali ya Dk. Mbwambo ambaye ni daktari bingwa wa matatizo ya wanaume (Mbwambo Dispensary) ambaye hakuwa na wauguzi wa kutosha, madaktari wasaidizi na baya zaidi tumemkuta na pakiti 10 za damu zilizokwisha muda wake.

Ina maana wagonjwa wakija anawawekea damu ambayo yeye aliibandika na plasta ili isionekane.”

Alisema tatizo hili linaonekana kubwa kutokana na waganga wakuu wa mikoa na wilaya kutofanya ukaguzi wao wa mara kwa mara na wa kina katika maeneo yao na kuwa wizara yake imejipanga kuwapa semina ya nini cha kufanya.

“Niitake jamii katika kushiriki kusimamia huduma za afya za umma na binafsi ili kuhakikisha ubora wa huduma, ukifika hospitalini jiulize kama imesajiliwa kwa kuangalia cheti ambacho kinatakiwa kuwapo Mapokezi na kama huduma wanayoitoa iko sahihi, maana ni lazima tulinde maisha yetu,” alisema.

Wakati huo huo, ikiwa kesho Tanzania inaadhimisha Siku ya Ukoma Duniani, tatizo la ugonjwa huo linaonekana kupungua kwa miaka 28 iliyopita kutoka kwa wagonjwa 35,000 mwaka 1983 hadi wagonjwa 2,600 mwaka 2009.

Akitoa tamko la maadhimisho hayo yanayofanyika Lindi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda alisema pamoja na kupungua kwa tatizo, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka jana, asilimia 11 ya wagonjwa wapya wamegundulika wakiwa wameshapata ulemavu wa kudumaa.

“Hii inaonesha kuwa walichelewa kwenda kwenye vituo vya afya kwa uchunguzi, na ugonjwa huu bado ni tatizo kubwa katika mikoa ya Lindi ambayo ina wagonjwa 176, Rukwa yenye wagonjwa 376, Dar es Salaam 386 na Mtwara wagonjwa 175 na kwa nchi nzima kuna wagonjwa 30,000 wenye ulemavu wa kudumu kutokana na ukoma.”

Alisema Serikali imejipanga kutokomeza ukoma kwa kutoa elimu kwa jamii, utoaji wa huduma katika kila kituo cha afya kwa kuhakikisha dawa zinapatikana na kwa wenye ulemavu imekuwa ikitoa huduma ya upasuaji, viungo bandia, magongo na viti mwendo.