WAZIRI wa Ujenzi, John Magufuli, amepiga marufuku ujenzi wa matuta kwenye barabara zote kuu nchini kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Pia ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kukagua na kusimamia miradi yote ya barabara za lami inayojengwa kwenye maeneo yao, tofauti na utaratibu uliokuwapo wa
miradi hiyo kukaguliwa na wataalamu wa makao makuu.

Magufuli alitoa maagizo hayo juzi alipozungumza na wafanyakazi wa Wizara hiyo mjini hapa, baada ya kukagua barabara ya Singida-Katesh wakati wa ziara yake ya ghafla ya siku moja.

Katika ziara hiyo pia alimwagiza mkandarasi anayejenga barabara ya Singida- Katesh - Sinohydro Corporation Limited ya China, kukamilisha kazi hiyo kwa wakati, vinginevyo Serikali haitaipa zabuni nyingine siku zijazo.

Kabla ya kutoa maagizo hayo, Kaimu Meneja wa Tanroads wa Mkoa, Joseph Masige, alisema ujenzi wa barabara hiyo uko nyuma kwani kazi iliyofanyika hadi sasa ni asilimia 51 tu badala ya asilimia 70 iliyopangwa.

"Ni kweli ujenzi unakwenda vibaya. Lazima mbadilike, mmalize kazi hiyo kwa wakati bila visingizio vyovyote, vinginevyo nitahakikisha hampati zabuni yoyote nchini.

"Kwanza mmelipwa fedha nyingi sana. Badala ya kununulia mitambo na zana mpya, nyie mnafanya mchezo wa kuhamisha vifaa hivyo kutoka mradi mmoja hadi mwingine kitendo kinachodhoofisha ufanisi wenu.

Hapa si mahali pa kuja kucheza," Waziri alimwonya mkandarasi huyo ambaye aliwakilishwa na Meneja Mradi huo, Xhinhua Chen.

Awali Chen alisema moja ya sababu za kuzorota kwa ujenzi huo ni kucheleweshwa malipo yao na Serikali suala ambalo Waziri aliahidi kulifanyia kazi.

Barabara ya Singida - Katesh yenye urefu wa kilometa 65.2 inafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa asilimia 60 na Serikali ya Tanzania asilimia 40 na inatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.