KATIKA kuonesha uungwana na ukomavu wa kisiasa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa niaba ya CCM na Serikali yake, amewaomba radhi viongozi wa dini nchini kutokana na kauli kinzani zilizotolewa na baadhi ya wagombea wa chama hicho mwaka jana.
Wagombea hao katika uchaguzi wa mwaka jana, walitoa kauli mbalimbali zilizokinzana na imani za dini zao.

Pinda aliwaomba radhi viongozi hao wa dini nchini kote jana kupitia kikao cha pamoja chake, viongozi hao na baadhi ya wazee maarufu wa hapa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Libori.

Alisema uchaguzi mkuu uliopita haukuwa laini kama ilivyotarajiwa … ulikuwa na changamoto nyingi zikiwamo tofauti za kimtazamo na kiimani, hivyo kwa yaliyojitokeza ya baadhi ya wagombea kugusa imani za dini za watu, halikuwa lengo lao kufanya hivyo na “tunaomba mtusamehe kwa yote yaliyojitokeza na kukwaza imani za dini zenu.

"Hali hiyo si kwamba ilijitokeza tu Sumbawanga ... najua tulimkwaza Mhashamu Baba Askofu (Damian Kyaruzi), tulikejeli imani ya dini yake, tunaomba radhi, mimi naomba radhi kwa
niaba ya CCM na Serikali.

“Si hapa tu lakini ni maeneo mengi nchini kama vile majimbo ya uchaguzi ya Hai na Same, ambako baadhi ya wagombea katika kuomba kura ya ndiyo walilazimika kutumia baadhi ya maneno yanayotumika katika Injili ya Mateso," alisisitiza Waziri Mkuu.

Alisema kutokana na hali iliyojitokeza CCM na Serikali wamepata fundisho, na katika uchaguzi ujao, aliomba viongozi wa dini, Serikali na vyama vya siasa, wakae pamoja kuweka angalizo ili wagombea wajiepushe na kejeli dhidi ya imani za dini za wengine na kuwasihi viongozi hao nchini kuanza ukurasa mpya na kutumia muda mwingi kuhamasisha maendeleo.

Akizungumzia rushwa, alikiri kukithiri katika uchaguzi mkuu huo na kuongeza kuwa ipo haja ya kuangalia upya mfumo wa uchaguzi kuanzia ndani ya CCM ambayo inajiandaa kwa uchaguzi wa viongozi wake mwakani kuhakikisha haitoi mianya ya rushwa na viongozi wa dini na wazee wakemee kwa nguvu zote rushwa.

"Rushwa ni rushwa tu, hakuna haja ya kusema kuna ndogo, hata mtu anapotaka kutimiza haja zake fulani kwa kutoa kitu kidogo ni rushwa ... pia kwa mgombea anapotoa doti ya khanga ili apigiwe kura, ni tatizo hivyo naiomba CCM ibadilike, najua ni jambo gumu lakini lazima tupigane nalo kikamilifu ... wagombea nao tabu tu, hasa kwenye chama safari hii tujirekebishe," aliasa.

Akishukuru, Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania Mkoa wa Rukwa, Mchungaji Israel Moshi, alisema madhebu ya dini yamesamehe, na viongozi wanapaswa kusamehewa, kwani wote ni binadamu na wanapaswa kusameheana kwa ajili ya maendeleo ya Rukwa na Taifa kwa jumla.

Akitoa mchango wake, Mhashamu Baba Askofu wa Anglikana Jimbo la Sumbawanga,
Marco Badeleya, alizungumzia Katiba mpya na kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kusikia kilio cha Watanzania juu ya kupata Katiba hiyo lakini akashauri kamati itakayoratibu upatikanaji wa Katiba hiyo, iundwe na watu waadilifu itakayoridhisha na kukidhi matarajio ya Watanzania.

Baadhi ya wachunguzi wa masuala ya siasa wameipongeza hatua ya Pinda kuwa muwazi na kukubali udhaifu kwa kuomba radhi na kusema hiyo ni njia ya kujenga utangamano katika jamii lakini pia kutambua mtu alikojikwaa na kujirekebisha.