BALOZI wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt amezitaka nchi za Afrika Kaskazini kuiga mfano wa Zanzibar katika kudai demokrasia, akisema anasikitishwa na mtindo wa nchi hizo kudai demokrasia kwa kumwaga damu.

Alikuwa akizungumza wakati wa hafla ya kumtangaza mshindi wa Tuzo ya Amani ya Dk. Martin Luther King kwa mwaka 2011 inayotolewa na Ubalozi wa Marekani ambayo imekwenda kwa Kamati ya watu sita ya kusimamia utekelezaji wa Azimio la Baraza la Wawakilishi kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Wajumbe wa kamati hiyo ambao kila mmoja alipata tuzo hiyo ni Mwenyekiti wake, Ali Mzee Ali kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abubakar Khamis Bakary (CUF) aliyekuwa Makamu Mwenyekiti na pia Kiongozi wa Upinzani Baraza la Wawakilishi na wajumbe Ali Abdalla Ali (CCM), Nassor Ahmed Mazrui (CUF), Haji Omari Kheir (CCM) na Zakiya Omari Juma (CUF).

Balozi Lenhardt alisema kamati hiyo ilisaidia kutoa elimu kuhusu uzuri na ubaya wa Serikali ya Kitaifa na kufanya watu wapige kura kwa amani ambapo zaidi ya asilimia 60 ya Wazanzibari walikubali kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi mkuu hivyo kuweka historia mpya Zanzibar.

“Tutadumisha kiwango cha juu cha misaada yetu katika maeneo muhimu na yanayowagusa watu wote, ambayo ni pamoja na elimu, afya, nishati na miundombinu. Mradi wa umeme wa megawati 100 kwenda Unguja utakamilika mwakani, mradi wa ujenzi wa barabara ya kilometa 35 huko Pemba huku jitihada zetu katika kuzuia na kutokomeza maradhi nazo zikiendelea,” alisema Balozi huyo.

Alisema, wakishirikiana na wadau wengine duniani katika nyanja ya teknolojia, wanafanya jitihada kupeleka kompyuta katika kila shule ya msingi visiwani Zanzibar na wiki hii atafungua shule mpya Bopwe na kliniki katika kambi ya Ali Hamisi huko Pemba.

Alisema, kuna changamoto kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutokana na masuala mengi magumu ya kutatua, ingawa ni matumaini yake Serikali hiyo ni hatua muhimu katika safari ya kuelekeza zama mpya na bora Zanzibar.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ali Mzee Ali alisema wanastahili kupata tuzo hiyo kutokana na kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inasimamia misingi ya haki na amani kama ilivyokuwa kwa Martin Luther King.

Alisema, katika kazi waliyofanya hawakuwalazimisha Wazanzibari kukubali Serikali ya Umoja wa Kitaifa ila waliwaeleza uzuri na ubaya wa Serikali hiyo, ambayo anasema itakoma pale wananchi watakapoamua.