Wasanii kutoka nyumba ya kukuzia vipaji vya sanaa (THT), Mzee Yusuf, Banana Zoro, Diamond, Linah na 20% ni baadhi ya wasanii nyota watakaopamba tamasha la utoaji wa tuzo za muziki za Kilimanjaro 'Tanzania Kili Music Awards 2011' zitakazofanyika Jumamosi kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
 Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia (TBL), David Minja, ambao ndio wadhamini wa tuzo hizo kupitia bia yao ya Kilimanjaro, alisema kuwa tamasha la mwaka huu litakuwa na tofauti kulinganisha na zilizopita kwavile limeboreshwa zaidi.
Minja alisema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilka na aliwataja wasanii wengine watakaotoa burudani siku hiyo kuwa ni C-Pwaa, Joh Makini, Ali Kiba, Diamond, Stara Thomas, kundi la Mapacha Watatu na burudani ya pamoja kutoka kwa washindi wa tuzo za Kili za mwaka uliopita.
Alisema kwa mwaka huu wanataka wananchi wapate nafasi ya kushuhudia tukio la utoaji wa tuzo hizo, hivyo tayari wameanza kuuza tiketi kwa watu watakaotaka kuhudhuria tamasha hilo.
Minja alisema kuwa lengo la kampuni yao kupitia bia ya Kilimanjaro ni kuhakikisha kuwa wanafikisha muziki wa Tanzania katika kilelele cha mafanikio.
Baadhi ya tuzo zinazoshindaniwa mwaka huu ni msanii bora wa kike, msanii bora wa kiume, mwimbaji bora wa kike na wa kiume, wimbo bora wa taarab, wimbo bora wa mwaka, wimbo bora wa kiswahili (bendi), wimbo bora wa Hip hop na rapa bora wa mwaka.