WAKATI Watanzania wakizidi kujitokeza kulaani maandamano ya kichochezi ya Chadema, familia ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, imeelezea kushangazwa na uongo wa viongozi wa chama hicho, kwamba familia hiyo inakiunga mkono.
Mbali na kuelezea kilichotokea wakati viongozi wa chama hicho walipotembelea familia hiyo hivi karibuni, pia imekemea mbinu za kutumia kaburi la Baba wa Taifa kujipatia umaarufu.

Kwa mujibu wa taarifa ya familia hiyo, tofauti na ilivyotangazwa na vyombo vya habari vinavyoshabikia maandamano hayo, familia hiyo haikuunga mkono maandamano hayo na badala yake ilisisitiza umuhimu wa kuzingatia utaratibu wa Serikali na kudumisha utulivu.

Akitoa taarifa hiyo jana, mmoja wa wanafamilia hiyo, Makongoro Nyerere, aliweka bayana kwamba familia hiyo haijaunga mkono Chadema kwa mambo inayoendelea nayo sasa, ikiwamo maandamano yaliyoendeshwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kwamba chama hicho kimepata baraka na kuombewa dua yenye lengo la kuungwa mkono na mjane wa Mwalimu Nyerere, Mama Maria na familia yake kwa lengo la kukitabiria ushindi.

Makongoro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mara, akifungua kikao cha Halmashauri ya CCM ya Mkoa kilichoshirikisha wajumbe na wabunge wa CCM wa mkoa huo, alisema kilichofanyika Butiama ni utaratibu wa kawaida wa kupokea wageni wanaotembelea kaburi la Mwalimu.

“(Viongozi wa Chadema) walipofika pale, kama kawaida mama (Mama Maria) aliwapokea na walimwomba kwenda kuzuru kaburi la marehemu baba, haikuwapo ajenda yoyote iliyoonesha kuwa Chadema walikuja pale ili waungwe mkono na familia yetu.

“Walikuja kuliona kaburi la baba, na ninachofahamu upo mchakato wa Kanisa Katoliki unaoendelea wa kumwandaa marehemu kuwa Mwenye Heri,” alisema na kuongeza kuwa haoni sababu ya watu kutumia kaburi la baba yake kujitafutia umaarufu.

Alifafanua kwamba kwa taratibu za Kanisa Katoliki, waumini wanaruhusiwa kushiriki kuombea mchakato huo ufanikiwe na Chadema ikiwa na baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki, familia iliona ni busara, mara baada ya ujio wao washiriki ibada ya maombi.

“Mama akiwa katikati yao kwenye kaburi la baba, aliomba juu ya watumishi wa Mungu kuendesha vyema mchakato huo ambapo pia alimshukuru Mungu kwa uchaguzi wa mwaka jana kufanyika kwa amani na utulivu … haya ya familia ya Mwalimu kuunga mkono Chadema yametoka wapi?

“Katika maombi yake, mama aliwakumbusha watumishi wote wa Mungu kutekeleza majukumu yao vyema bila ya kukiuka taratibu, sikuona mahali alipotamka suala hilo,” alisema huku akionesha kushangaa.

Mkoani Dar es Salaam, taasisi ya Tanzania Rural and Urban Youth Alliance (TRUYA), inayokutanisha vijana waliopo shuleni, vyuoni, mijini na vijijini, imewataka wanaoeneza chuki baina ya wananchi, Serikali na vyombo vya usalama kuacha mara moja.

Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo iliyotolewa Dar es Salaam jana, suluhu ya matatizo si kuchafuana kwa maneno makali au kudharauliana kwa namna yoyote ile.

Taasisi hiyo imehadharisha kuwa machafuko yanayoendelea barani Afrika kama vile Tunisia, Misri, Libya na Ivory Coast, si ya kuigwa, kwa sababu yanaweza kuhatarisha usalama na amani ya nchi na kusababisha machafuko na uvunjifu wa haki za binadamu.

Mwenyekiti wa Truya, Herman Shelutete, katika taarifa hiyo aliwataka wananchi kushauriana jinsi wanavyoweza kuinusuru nchi isiingie katika machafuko na uvunjifu wa amani.

“Katiba ya nchi ibara ya 18 inatambua haki ya mtu kutoa maoni na kusikilizwa, haki ya kuandamana kwa amani na kwa mujibu wa sheria. Pale sheria zinapovunjwa ili kupata haki hizo ni kuhatarisha amani ya nchi na hatuna budi kukemea vitendo hivyo kwa nguvu zote,” alisema Shelutete.

Mkoani Morogoro, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alitoa onyo kwa wanawake kuacha kushabikia na kushiriki maandamano ya Chadema.

Katika onyo hilo, Simba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), alifafanua kwamba maandamano hayo yanalenga kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani na lengo hilo likitimia, watakaoathirika zaidi ni wao na watoto.

Akitoa hotuba yake ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka juzi mjini Ifakara, Waziri Simba aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alisisitiza kuwa ni makosa kwa wanawake kushabikia vurugu au kushiriki maandamano hayo.

“Mbinu za Chadema na vibaraka wao akina mama tumezishitukia, tusikubali kuingizwa kwenye mkumbo huu, wanatumia maandamao ili kutaka kufuta historia nzuri ya amani na utulivu uliojengwa na Mwalimu Nyerere, inayosifika duniani kote,” alisema.

“Fujo hizi hazitawafungulia mlango wa Ikulu abadan … Ikulu mtu anakwenda kwa ridhaa yetu sisi wananchi hasa wanawake, na tayari wananchi na sisi wanawake tumemchangua Jakaya Kikwete kupitia CCM kuwa Rais wetu…kinachohitajika sasa ni kuhubiri maendeleo ya wananchi,” alisema Simba.