Watu 10 wamejeruhiwa na wengine 66 hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuezuliwa mapaa na nyingine kuanguka kufuatia mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kunyesha katika kitongoji cha Mwayunge mjini Igunga mkoani Tabora.

Walioshuhudia wamesema mvua hiyo ilianza saa 3:00 usiku wa kuamkia jana na kwamba mbali ya maafa hayo, pia imesababisha uharibifu mkubwa mashamba na samani zilizokuwamo ndani ya nyumba hizo.
Walisema waliojeruhiwa walikuwa wakijaribu kuokoa baadhi ya mali zao huku mvua hiyo ikiendelea kumwagika.
“Baada ya mvua hiyo kuanza kunyesha, watu wengi tulishikwa na kiwewe na kukimbia huku na huku pasipo kujua tunakoelekea,” alisema mmoja wa waathirika hao, John Nakimbata.
Afisa Tawala wa Wilaya ya Igunga, Kigatta Anthony, alisema kati ya watu 10 waliojeruhiwa, watano hali zao ni mbaya na walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga kwa matibabu.
Aidha, alisema waathirika hao ni jumla ya familia 13 ambapo saba kati yake, zimepata hifadhi kwa ndugu zao eneo la mjini hapa na sita zinaendelea kuishi hapo wakati utaratibu wa kuzisaidia ukiendelea.
Baadhi ya waathirika hao walisema mvua hiyo imewaweka katika hali ngumu ya kimaisha kwani hawajui pa kuanzia kutokana na kuharibikiwa na vitu vyao na hasa akiba ya chakula.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Dk. Kisilla, alisema majeruhi wote waliopokelewa hospitalini hali zao zinaendelea vizuri na tayari wameruhusiwa wote kwenda makwao.