Viongozi kadhaa kutoka nchi za Afrika, ikiwemo Uganda, Afrika Kusini na Zimbabwe, wamelaani mashambulio ya angani nchini Libya.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameandika makala ndefu kwenye gazeti akizishutumu nchi za magharibi kwa kuwa ndumilakiwili.
Alikuwa ni mmoja miongoni mwa viongozi watano wa Afrika waliopewa jukumu la kutafuta suluhu la mgogoro Libya, ambapo safari ya ujumbe huo mjini Tripoli uliahirishwa baada ya mashambulio kuanza.
Bw Jacob Zuma wa Afrika Kusini naye alikuwepo kwenye jopo la Umoja wa Afrika.
Licha ya Afrika kusini kupiga kura ya azimio la umoja wa mataifa mwaka 1973, iliyoidhinisha hatua za kijeshi kulinda raia, Bw Zuma naye amelaani mashambulio hayo ya anga, akisema ni sehemu ya "sera za mabadiliko ya uongozi."
Viongozi wa nchi za magharibi walisema mashambulio hayo hayatomlenga kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi lakini wanataka aachie madaraka.
Bw Zuma alitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano haraka iwezekanavyo na "kukataa kuingiliwa na nchi yeyote ya kigeni, hata iwe katika muundo upo".
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, mkosoaji mkuu wa nchi za magharibi, naye amelaani mashambulio hayo ya anga, akisema mgogoro wa Libya ni kuhusu utajiri wake wa mafuta.
Hifikepunye Pohamba, Rais wa Namibia naye amekubaliana na hilo, akiita shambulio hilo ni "kuingilia masuala ya ndani ya Afrika."
Umoja wa Afrika nao umetoa wito wa kumaliza uvamizi wa kijeshi nchini Libya.