MUIGIZAJI mahiri wa kundi la Orijino Komedi, Masanja Mkandamizaji, mwishoni mwa wiki iliyopita aliteka mkutano wa Injili kwenye viwanja vya Ubungo External, Dar es Salaam.
Masanja ambaye jina lake halisi ni Emmanuel Mgaya pia ni muimbaji wa nyimbo za Injili na msanii aliyeokoka alialikwa kupamba mkutano huo, lakini uwepo wake ulionekana kuvuta hisia za wasikilizaji wengi zaidi. Baada ya Mchungaji Bupe Kingu ambaye ni mke wa Nabii Moses Kingu mwenyeji wa mkutano huo wa mwezi mmoja uliokuwa ukifanyika kwenye viwanja hivyo kutangaza Masanja kupanda jukwaani umati wa watu ulishangilia na waliokuwa mbali wakaanza kusogea eneo la mkutano.

Hali hiyo iliamsha hisia za wasikilizaji wengi na kushangilia wakionekana wazi kufurahia uwepo wa Masanja na shauku ya kumuona.

Masanja ambaye alijiita Mchungaji mtarajiwa alipanda jukwaani na kuimba wimbo wake wa 'Nimeamua Kumfuata Yesu' na kuwataka watu wote kucheza.

Baada ya wimbo huo pia alishirikiana na mwanamuziki nyota wa Injili, Christina Shusho katika kibao cha 'Unikumbuke'.

Masanja aliwapasha watu wanaohoji kama ameokoka na kusema: “Hivi kwa nini watu wanajiuliza Masanja kaokoka kweli, kabla hujajiuliza anza kujiuliza wewe umefuata nini.”

Masanja aliuhakikishia umati huo kuwa yeye ameokoka. “Ujanja ni kuokoka, wajanja wote wamekimbilia kwa Yesu. Mtake msitake ndivyo ilivyo.”

Mchungaji Bupe alisema kuna watu wamekuwa wakimtumia ujumbe wa simu kuhoji kualikwa Masanja kwenye Mkutano wa Injili na baadhi kubeza wasimchezee Mungu.

“Kuna watu wamekuwa wakituma ujumbe kwenye simu wakihoji kama Masanja ameokoka na kusema tusimchezee Mungu. Yeye mwenyewe yupo hapa na mtasikia kutoka kwake,” alisema.