Rashidi Nyamugwalela Warioba (aliyevaa shati mikono mirefu) akifanyiwa mahojiano na mwandishi wa makala haya wilayani Nachingwea.RASHID Nyamugwalela Warioba ni mzaliwa wa kijiji cha Marembeka, wilayani Bunda Mkoa wa
Mara.
Lakini amehamisha makazi kwa ajili ya kujitafutia riziki, na sasa ni mkazi wa kijiji cha Ikungu Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi; akijishughulisha na biashara za uchimbaji wa madini aina ya dhahabu. Warioba aliyezaliwa mwaka Desemba 23, 1964 aliamua kutafuta maisha , kwa kuanza kufanya biashara ya kuuza maji, kuni, samaki na nguo machimboni Nachingwea.

Aliendelea na biashara hiyo kwa muda, kabla ya mwenyewe kuamua kujikita kwenye machimbo moja kwa moja na sasa anamiliki machimbo yake, yenye ukubwa wa hekta 19.8 yaliyoko katika kijiji cha Ikungu.

Zaidi ya watu 200 katika kijiji cha Ikungu wanapata ajira katika mgodi huo uliopo umbali wa kilomita sita kutoka mjini Nachingwea. Machimbo ya Ikungu yanazungukwa na vijiji vinne ambavyo ni Rupota, Malambo Ikungu na Malamba wilayani Nachingwea.

Umiliki wa mgodi huo aliupata kutoka Wizara ya Nishati na Madini Oktoba mwaka jana. Anasema kwamba mpaka kufikia kumiliki mgodi huo alisota kwa kufanya kazi nyingi, ambapo wateja wake wakubwa wakiwa ni akinamama lishe.

Ndoo ya kwanza ya kuuzia maji alipewa na mama mmoja ambaye alikuwa anatoka Mwanza na ataikumbuka kama kifaa kilichoanza kumwingizia fedha, akiitumia kusombea maji. Baada ya kuuza maji hatimaye alifanikiwa kununua ndoo ya pili, ambapo anakumbuka alichukua mti aliokuwa akiuweka kwenye bega lake na kufikisha machimboni.

Warioba anasema kwamba alifanikiwa kununua baiskeli, kwa hiyo akaanza kufanya kazi za usiku kusomba maji ili mama lishe wanapofika asubuhi wakute tayari maji yapo kwa ajili ya matumizi ya kupikia vyakula vya biashara.

Anasema kwamba licha ya kuuza maji, aliendelea kufanya biashara ya kukata kuni na kujipatia samaki kwa ajili ya kuwauzia mama lishe hao waliotokea kuwa soko lake kubwa katika machimbo hayo.

Warioba anasema kwamba alifika wilayani Nachingwea mwaka 1997 baada ya kuwa amepewa fedha za kufanyia biashara ya kuuza mbuzi Vingunguti na mzee aliyemlea aitwaye Webiro Mkama.

Mzee huyo alimchukua mnamo mwaka 1996 baada ya kumalizika uchaguzi wa mwaka 1995, mzee mwenyewe akiwa Mwenyekiti kitongoji cha Liyamungali, kijiji cha Kurusanga, wilayani Bunda.

Anasema kwamba baada ya mzee huyo kuwa Mwenyekiti awali alikuwa na nia ya kumwendeleza Warioba kielimu, lakini mwenyewe akakataa, hivyo akaomba apewe fedha kwa ajili ya kufanya biashara.

Warioba anasema kwamba alipewa Sh 300,000 kwa ajili ya kufanyia biashara ya kuuza mbuzi eneo la Vingunguti Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam. Hata hivyo, alijaribu lakini biashara
hiyo ikashindikana, ndipo akaamua kununua nguo na kwenda kuziuza Nachingwea.

Biashara haikuwa nzuri huko, naye akaamua kubaki hapo hapo Nachingwea, na huo ulikuwa mwaka 1997. Anakumbuka jinsi hali ilivyokuwa ngumu kimaisha, kutokana na ukweli
kwamba mtaji aliokuwa nao uliisha, ndipo akaamua kubuni biashara nyingine.

Hiyo haikuwa nyingine, bali ya kuuza maji, baada ya kusikia kuna machimbo ya Ikungu. Warioba anasema alifanya kazi hiyo mpaka mwaka 2000 alipopata kazi kwenye kampuni ya utafiti ya Golo Mine Enterprises.

Alisema kampuni hiyo ilikuja kubadilishwa jina kuwa Ikungu Mine, na ilipofika 2009, aliomba
leseni ndogo iitwayo (primary mine license) iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini, mjini
Dar es Salaam Oktoba mwaka jana.

Sasa mambo yake yanakwenda vizuri, kwani anatoa ajira kwa watu zaidi ya 200 kwenye mchimbo matatu aliyo nayo. Mashimbo hayo yenye mita 120 na madini yanayochimbwa zaidi ni dhahabu.

Anaongeza kwamba licha ya kumiliki aneo hilo, anamiliki mashine aina ya kompresa kusaga
mawe na kusafisha dhahabu. Kuna wakati alikuwa analala machimboni kutokana kutokuwa
na nyumba wala uwezo wa kupanga, lakini sasa anaishi kwake, akiwa pia na mke na watoto.

Anasema makusanyo ya dhahabu hupanda au hushuka kutegemeana na jinsi ya wafanyakazi wanavyoweza kukusanya. Anatoa mfano kwamba Desemba 13 mwaka jana alipata gramu
11, Desemba,19 akapata gramu 15.2, Desemba 20 akapata gramu 19.8, wakati Desemba 23 zilikuwa gramu 46.1 huku Februari mwaka huu akijipatia gramu 11.1.

Anasema ana nyumba Bunda, ng'ombe zaidi ya 100 na nyumba na maduka ya dawa wilayani
Nachingwea. Anasema kwamba ili aweze kumshukuru Mungu anatafuta kiwanja ili ajenge kanisa wilayani Nachingwea, ambapo waumini watapata fursa ya kumwabudu Mungu wao.

Anatoa mwito kwa jamii isikate tamaa kimaisha, bali izidi kujituma kwa kutumia mtaji, na kwa watu masikini, anasema kwamba mtaji wao ni nguvu zao wenyewe. Kimaisha, anaeleza, kuna
changamoto nyingi zinazohitaji watu kuwa wavumilivu kila wakati, ili wapate kufanikiwa
katika maisha.

Warioba anasema kwamba mama yake mzazi ni Mose Kinanda wakati baba yake ni mzee
Nyamwugwalela ambaye alifariki kabla Warioba hajazaliwa. Alipata elimu ya msingi aliyohitimu mnamo 1981, akiwa anakaa kwa mjomba wake, mzee Masembo Kinanda,
wilayani Magu Mkoa wa Mwanza.