MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, amelaani kitendo cha mauaji ya polisi wawili yaliyofanywa na majambazi mkoani Shinyanga Jumatano iliyopita.
IGP Mwema alisema, Jeshi la Polisi halitaweza kuvumilia vitendo kama hivyo viendelee kutokea mahala pengine popote hapa nchini.
Hata hivyo, IGP Mwema alipongeza juhudi za wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine jirani kwa ushirikiano wao uliofanikisha kukamatwa kwa majambazi sita kati ya kumi waliopora silaha ya polisi na kuwaua askari Polisi wawili katika kituo kidogo cha Kagongwa wilayani Kahama na kukimbia. IGP Mwema alikuwa akifunga mkutano mkuu wa mwaka kwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi uliokuwa ukifanyika katika Chuo cha Taaluma za Polisi kilichopo mjini hapa.

Alisema ushirikiano huo ukidumishwa katika maeneo mbalimbali, utaliwezesha Jeshi la Polisi kuendeleza bila kuchoka mapambano dhidi ya uhalifu hapa nchini.

IGP alisema kuwa juhudi za kuwatafuta majambazi wengine wanne zinaendelea na kwamba tayari zimeonesha dalili za mafanikio na muda si mrefu watuhumiwa hao watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria kujibu tuhuma zao.

Wakati wa mkutano huo, maofisa hao wakuu wakiwemo makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi pamoja na watumishi raia wa Jeshi hilo, wameweka maazimio manane ambayo yanalenga katika kusimamia nidhamu na maadili ndani ya Jeshi hilo.

Miongoni mwa maazimio hayo pia ni kuimarisha usimamizi wa rasilimali za Jeshi la Polisi pamoja na kubaini matishio ya Usalama wa Taifa la Tanzania.

Pia walipendekeza kuimarisha matumizi ya mifumo ya mtandao wa kompyuta katika utendaji wa kazi za Polisi hasa kwenye nyanja za Upelelezi wa Makosa ya Mitandao na kuboresha mawasiliano.

Aidha alisema kuwa mifumo hiyo itasaidia kujenga uwezo kwa wapelelezi watendaji katika kufanikisha masuala ya upelelezi na usimamizi wa kesi na upatikanaji wa taarifa za wahalifu.

Aliwambia makamanda hao kuwa ni muhimu kwa kila kiongozi katika ngazi zote kuanzia ngazi ya Kituo, Wilaya, Mkoa hadi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwenda kutoa elimu ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano huo.

IGP Mwema alisema kuanzia sasa kila askari, mkaguzi na ofisa ni lazima awe ni sehemu ya suluhisho la matatizo yanayowakabili katika himaya zao na kinyume cha hivyo basi mtendaji huyo ndiye atakuwa sehemu ya tatizo husika.

Wakati wa mkutano huu pia, washiriki walipata fursa ya kutambua matishio ya usalama na kuibuka kwa aina mpya za uhalifu hapa nchini.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kamishna Robert Manumba, aliwataka Makamanda hao wa Polisi wa Mikoa, mara warudipo katika vituo vya kazi, wakahakikishe kuwa, wanapata nafasi ya kuwasikiliza wananchi na kupokea mawazo na ushauri wao ili kuwawezesha kupata kukabiliana na uhalifu ukiwemo wa majambazi wenye silaha.

Kamishna Manumba alisema kuwa kama kila kamanda atakuwa karibu na wananchi, itakuwa rahisi kwao kupata taarifa za kihalifu pamoja na nyendo za watenda makosa.

Mkutano huo wa siku tatu ambao ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, uliwashirikisha maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi pamoja na watumishi raia wa Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo pia walikuwa wakiangalia changamoto na mafanikio kwa mwaka uliopita na kupanga mikakati mipya ya kukabiliana na wimbi la uhalifu hapa nchini.