Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), wameitaka serikali kufunga viwanja vya ndege vilivyojengwa katika maeneo ya migodi kwa kuwa vinatumiwa na wawekezaji kutorosha dhahabu nje ya nchi bila kulipa mapato.
Wamesema hakuna haja ya makampuni ya madini kuwa na viwanja maeneo ya migodini, badala yake watumie viwanja vikubwa vilivyopo nchini wakati wakisafirisha dhahabu ili iwe rahisi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya mapato.
Akichangia katika kikao kati ya Wizara ya Nishati na Madini na wajumbe wa kamati hiyo, kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, alisema ana ushahidi kwamba, wawekezaji wanatorosha dhahabu nje ya nchi kwa kutumia viwanja wanavyomiliki maeneo ya migodini.“Mheshimiwa Mwenyekiti, hili sio jambo la siri. Hawa wawekezaji wanatumia viwanja hivi kuvusha dhahabu kwa kutumia ndege zao, ambazo hazipiti kwenye viwanja vya kawaida,” alisema.
Alisema serikali wamekuwa wepesi kufanya ukaguzi katika mazao ya pamba, ambayo yanasafirishwa nje ya nchi kwa kukagua kontena moja baada ya lingine, lakini kwenye madini wameshindwa kufanya hivyo ingawa huko ndiko kwenye fedha nyingi.
Masele alisema pia ana mfano hai kwamba, mgodi wa Mwadui, mkoani Shinyanga ingawa hivi sasa umefungwa, wawekezaji wanafanya uzalishaji kinyemela, huku wakikwepa kulipa mapato ya serikali.
Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim Issa, akichangia katika kikao hicho, alisema wawekezaji ni watu waliokuja kuchuma, hivyo sio watu wa kuaminiwa, wafanyekazi nwenyewe bila kusimamiwa na kisha waweze kulipa mapato sahihi.

Aliitaka serikali kuwafuatilia na kuwabana badala ya kuwafanyia uzembe na kuwaacha wakichota dhahabu nyingi bila kulipa mapato halisi ya serikali.
Kamishna wa Madini wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk. Peter Kafumu, alipingana na hoja hizo na kusema ndege zote zinazochukua vifurushi vya dhahabu zinapitia kwenye Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Kilimanjaro (KIA) na Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam. Alisema katika viwanja hivyo, kuna maofisa wa TRA na wa madini, ambao wanahakikisha mzigo wote umekaguliwa kabla ya kuondoka nchini.
Hata hivyo, Dk. Kafumu aliwashangaza wabunge baada ya kusema kuwa wawekezaji wakubwa ni watu wema na waaminifu na kwamba wanaoweza kufanya uhuni kama huo, ni wachimbaji wadogowadogo, ambao ni wazawa kwa madai ya kugopa kufungiwa biashara zao kwenye soko la hisa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zainabu Vulu, alimtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, kutoa msimamo wa serikali kuhusu madai ya wabunge hao, ambapo alisema amepokea mawazo yao na atayafanyia kazi. Akitoa taarifa ya mapato ya serikali yanayotokana na madini, Jairo alisema ukusanyaji wake ni mzuri na ndiyo sekta inayoongoza kwa mapato kuliko wizara nyingine.