Mlinzi wa Manchester United Rio Ferdinand huenda asicheze msimu wote huu uliosalia kutokana na jeraha la msuli.
Nahodha huyo wa England alipata majeraha wakati wa mazoezi kabla ya mchezo dhidi ya Wolves Februari 5 mwaka huu.
Meneja Sir Alex Ferguson amesema: "Tunatazama jambo hili kama la muda mfupi - tutakuwa na bahati kama Rio atarejea kabla ya kumalizika kwa msimu."
United imepata pigo zaidi baada ya taarifa za mlinzi John O'shea kutoweza kucheza kwa wiki tano kutokana na tatizo la misuli ya paja.
Nahodha Nemanja Vidic hatocheza mechi dhidi ya Bolton siku ya Jumamosi kutokana na jeraha la msuli wa mguu, na hivyo walinzi waliopo kwa sasa ni - Fabio, Chris Smalling, Wes Brown na Patrice Evra.
"Vidic hatocheza - anaonesha dalili nzuri za kupona wiki hii, na atakuwa tayari baadaye, lakini siyo Jumamosi," amesema Ferguson.
Meneja huyo pia amethibitisha kuwa Rafael huenda asicheze kwa "wiki mbili au tatu" baada ya mchezaji huyo kutoka uwanjani akichechemea, kwenye mchezo dhidi ya Marseille.
Ferguson amesema huenda akamchezesha Jonny Evans, ambaye hajacheza tangu mechi dhidi ya Wolves.
"Umekuwa wakati mbaya kwetu," amesema Ferguson.