WANASIASA wameanza kupageuza Loliondo kwa Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwaisapile, kuwa mtaji wa kisiasa.
Hali imefikia hatua hiyo kutokana na mlolongo wa wanasiasa hao wakiwamo wabunge, kupeleka idadi kubwa ya wagonjwa kwa gharama kubwa kwa Mchungaji huyo maarufu kama Babu.Baadhi ya wanasiasa hao ni Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema), Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), Mbunge wa zamani wa Musoma Mjini, Vedastus Manyinyi (CCM), Godbless Lema wa Arusha (Chadema), na Aeish Hilaly (CCM) wa Sumbawanga Mjini. Baadhi ya wanasiasa hao ni Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema), Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), Mbunge wa zamani wa Musoma Mjini, Vedastus Manyinyi (CCM), Godbless Lema wa Arusha (Chadema), na Aeish Hilaly (CCM) wa Sumbawanga Mjini.

Wengine ni Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM) na wa Rorya, Lameck Airo (CCM) aliyejitolea kupeleka watu 150.

Akizungumza jana na mwandishi wa habari hizi mjini hapa, Lema alisema ametenga Sh milioni 12 kwa ajili ya kusafirisha watu 200 kwenda Loliondo kunywa dawa.

Amefanya hivyo baada ya kupata ushuhuda wa marafiki zake, wabunge na majirani kwamba wagonjwa watumiao dawa ya Mchungaji wanapona.

"Nitakuwa sijawatendea haki wananchi wa jimbo langu kama msaada wa uponyaji unapatikana mkoani kwangu, halafu nishindwe kuwasaidia, ndiyo maana nimetenga fedha hizo, kwa ajili ya kusaidia wananchi wangu ambao hawana uwezo wa kwenda huko," alisema.

Kwa upande wake, Nyangwine naye alisema amejiandaa kupeleka wananchi 200 ambapo amewataka wajiorodheshe ofisini kwake tayari kwa safari hiyo.

"Nimeamua kupeleka baadhi ya wapiga kura wangu ambao wanajisikia kuumwa wakapate tiba kwa Babu kama shukurani zangu kwao kwa kunipa kura zilizonipa ushindi na kulikomboa jimbo la Tarime kutoka Chadema na kurejesha amani na sasa wananchi wanachapa kazi za maendeleo," alisema Nyangwine.

Wakati huo huo, wananchi wanaokwenda Loliondo kunywa dawa ya ‘Babu’, wameiomba Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya mapato kutokana na watu wa nchi mbalimbali kufika eneo hilo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, wananchi hao walisema wakiwa Loliondo wameshuhudia helikopta kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda na magari ya nchi hizo yakiwa kwenye foleni kusubiri dawa na abiria wao.

Mmoja wa wananchi hao, Prosper Lyaruu kutoka Dar es Salaam, aliyedai amekuwa akisumbuliwa na kiuno na kuvu kwenye miguu na baada ya kupata kikombe cha dawa amepona, alisema nchi inakosa mapato kutokana na kukosekana kwa Idara ya Uhamiaji na TRA wilayani hapo.

Lyaruu alisema umati katika eneo hilo ni mkubwa ukijumuisha raia kutoka nchi mbalimbali, lakini hakuna idara yoyote ya Serikali inayokusanya mapato kutokana na matibabu ya Babu huyo.

Alisema endapo Uhamiaji na TRA watahamia kwa muda Loliondo, nchi itapata mapato kwani helikopta zinapeleka baadhi ya wagonjwa katika eneo hilo tena raia wa kigeni bila hata vibali vya kisheria ; lakini pia kuna biashara inafanyika eneo hilo.

Imelda John alisema Loliondo kuna mambo mengi ikiwa ni pamoja na uhaba wa mawasiliano kwani hivi sasa ni mtandao wa Airtel pekee ndio unaopatikana tena kwa kwenda kwenye nyumba ya mkazi wa eneo hilo, ambaye anatoza mtumiaji wa simu Sh 500 kwa kutumia eneo lake kupata mawasiliano.

Aliongeza kuwa hivi sasa utaratibu wa kunywa dawa ni mzuri na mtu anaweza kwenda leo akarudi kesho yake na kuendelea na mambo mengine ila alisisitiza akaunti ya Babu ianzishwe ili watu wachangie fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya wilaya hiyo ikiwamo upatikanaji maji safi na salama, makazi mazuri ya watu wanaokwenda kupata huduma na vyoo vya kutosha.