SERIKALI imeliagiza Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lianze kujenga Daraja la Kigamboni, Dar es Salaam, ili kurahisisha usafiri kwa wakazi wa maeneo ya Kigamboni na jirani zao.
Daraja hilo linatarajiwa kutumia zaidi ya Sh bilioni 130 hadi litakapokamilika, NSSF itatoa Sh bilioni 100 na Serikali Sh bilioni 30.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, ametoa agizo hilo leo Dar es Salaam baada ya kutembelea eneo la Kurasini Vijibweni, Dar es Salaam ambako daraja hilo linatarajiwa kujengwa.
"Tumezungumza siku nyingi kuanza ujenzi wa daraja la Kigamboni, ifike wakati tuanze, kwani Serikali haiwezi kukosa asilimia 40 ya fedha zinazohitajika kukamilisha ujenzi huo," alisema Magufuli.Amesema, katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, Serikali itajitahidi kutafuta fedha ikiwamo kutenga katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi, ili kuhakikisha ujenzi wa daraja hilo unakamilika kabla ya uongozi wa awamu ya nne kumaliza muda wake ambazo ni sawa na Sh bilioni 100 ambazo zinatosha kuanza ujenzi wa daraja hilo wakati Wizara ya Ujenzi ikitafuta zaidi ya Sh bilioni 30 zilizobaki ili kukamilisha ujenzi

"NSSF nawaomba mjitahidi kukamilisha taratibu zote na kisha wiki ijayo (Ijumaa ) mtangaze zabuni ili ikiwezekana ujenzi uanze mara moja ... ili likikamilika, litusaidie katika kupunguza msongamano katikati ya Jiji, kwani feri zitaanza kusafirisha abiria kwenda Tegeta na Bagamoyo badala ya kutumia barabara," amesisitiza Dk. Magufuli.

Amesema, kimsingi NSSF kutokuwa na asilimia 100 za fedha zinazohitajika katika ujenzi wa daraja hilo, hakuwezi kuwafanya wasianze mradi, kwa kuwa katika mradi wowote, mkandarasi anaanza kwa kulipwa fedha kiasi na kisha anaongezwa kulingana na anavyoondelea na mradi.

Dk. Magufuli amesema, ujenzi huo ni muhimu kwa kuwa eneo hilo lina wananchi wengi wanaofanya kazi katikati ya Jiji, hali kadhalika kuna miradi mingi inayotarajiwa kuanzishwa ukiwamo ujenzi wa kituo cha mabasi yaendayo Mtwara na Lindi na kuwapo kwa viwanja 10,000 vya NSSF.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Crescentius Magori, alisema, shirika hilo hadi sasa ina Sh bilioni 100 kati ya Sh bilioni 130 zinazohitajika, kukamilisha ujenzi huo haraka.

Alisema, daraja hilo litakuwa na njia nne za magari na mbili za watembea kwa miguu.

Magori alimhakikishia Magufuli, kuwa watajitahidi kutangaza zabuni wiki ijayo mara baada ya kuhakikishiwa kuwa Serikali itachangia asilimia 40 ya gharama za ujenzi wa daraja hilo linalotarajia kuchukua miaka mitatu kukamilika