MALEZI YA WATOTO WETU  NA ULAYA
 
Kama mnavyoona kichwa cha habari hapo juu,malezi ya watoto wetu na ulaya.Inafahamika ya kwamba malezi ya mtoto si jambo rahisi lakini kwa ulaya kwa sisi wazazi wa kiafrika huwa ni maradufu.Nitazungumzia zaidi juu ya suala la kimaadili zaidi na sio la kifedha.
 
Kama ilivyo ada mtoto anahitaji kufundishwa maadili mema toka akiwa na miaka miwili au chini ya hapo mpaka ukubwani mwake na hili suala kwa nyumbani ni suala la jamii nzima likongozwa na wazazi wa mtoto.kinyume chake suala la kumlea mtoto ni la wazazi tu hapa ulaya na hilo linatuwia vigumu sana sisi ambao tulishazoea mfumo wa nyumbani.
 
Maadili ya malezi na maisha kwa ujumla ni tofauti kati ya waafrika na wazungu.utakuta wazazi wengi hapa ulaya wanaiga malezi ya kizungu wakati watoto wao wakiwa wadogo(ambayo hawayajui kiundani kwa sababu wanayaona kwa nje tu) na kutegemea mtoto awe na adabu za kiafrika akishakuwa msichana au mvulana,wakati huo tumesahau ule msemo "usemao mtoto umleavyo ndivyo akuavyo" na matokeo yake huwa kinyume na matarajio ya wazazi  kwani mtoto anakuwa ameshaharibika.Hii yote inatokana na mzazi kumchanganyia mtoto staili ya maisha ya kizungu na kiafrika na matokeo yake mtoto hajui wapi pa kushika na kuamua kuunda stahili yake anayoijua mwenyewe ambayo ni maharibiko.
 
Kama nilivyosema hapo juu mtoto ni wa jamii nzima lakini hapa ulaya mtoto ni wa wazazi tu kwa hiyo sisi wazazi wa huku ulaya tuna kazi ya ziada katika kuwafundisha watoto wetu maadili mema ambayo yatawasaidia baadae na si kuuachia uilmwengu utufundishie kama dhana za wazazi wengine ambao wanaona mtoto akienda shule na akifanya kazi za shule nyumbani basi kamaliza na mengineyo atafanya vile anavyotaka na anavyojua au kuwaiga wazungu wanafanya vipi kwa kuwaona nje au kwenye filamu.kawaida wazungu wana maadili yao na mikakati yao juu ya malezi ya watoto wao lakini ieleweke maadili ya kizungu si maadili yetu kwani kuna tofauti kubwa sana juu ya mila na desturi zao na zetu.
 
Kuna usemi usemao "mtoto akiongoka ni furaha ya wazazi" na hakuna mzazi asiyependa kumuona mwanae ameongoka.Kama alivyosema bwana mmoja mtukufu kabisa katika falsafa amani iwe juu yake kwamba "hakutoa zawadi mzazi kumpa mwanae zawadi iliyo bora kama kumfundisha tabia njema".
                                                  (Itaendelea jumamosi ijayo) Tunaomba maoni na ushauri au maswali juu ya maisha ya Ulaya,tupo kwa ajili yenu kwa kuisaidia na kuifundisha jamii masuala ya ulaya kwa ujumla.Tuonane wiki ijayo....