Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limesema hali ya umeme katika mikoa inayopata nishati hiyo kutoka Gridi ya Taifa imeboreka kidogo, baada ya maji ya mvua za masika zilizonyesha katika baadhi ya mikoa nchini hivi karibuni, kuingia katika mabwawa manne na hivyo kupunguza makali ya mgawo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando(Pichani), alisema jana kuwa kuboreka kwa hali hiyo, pia kunatokana na mitambo ya kuzalisha umeme ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kuongeza uzalishaji wa nishati hiyo kufikia megawati 60 kwa sasa.
Mabwawa hayo ambayo alisema maji ya mvua hizo yaliingia na hivyo kuleta unafuu katika mgawo wa umeme ulioikumba mikoa hiyo, ni pamoja na Kidatu, Kihansi na Nyumba ya Mungu.