Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imeongeza muda wake kwa mwaka mwengine mmoja licha ya kukosolewa na wafadhili na mashambulio kutoka kwa wapiganaji.
Serikali ya Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, aliyekuwa mwasi wa msimamo wa kati, alitarajiwa kuachia madaraka mwezi Agosti 2011.
Tangazo hilo limetolewa baada ya wabunge wa Somalia kujiongezea muda wa kukaa kwa miaka mingine mitatu.

Wapiganaji wa kiislamu wanaoshirikiana na al-Qaeda wanadhibiti eneo kubwa la nchi hiyo.
Lakini serikali hiyo, inayoungwa mkono na jeshi la Umoja wa Afrika, limeweza kudhibiti maeneo kadhaa hivi karibuni kwenye mji mkuu, Mogadishu kutoka kwa kundi la al-Shabab.
Serikali hiyo, iliyotikiswa na mgawanyiko wa ndani kwa ndani, imesema isingewezekana kufanya uchaguzi uliokuwa ukitarajiwa kufanyika mwezi Agosti.
Wafadhili wa nchi za magharibi, wanaoisaidia serikali hiyo kifedha, wamelaani hatua hiyo hivi karibuni.
Bunge lililopo sasa lilichaguliwa wakati wa mkutano wa amani mwaka 2004.
Somalia haijawa na serikali ya kitaifa madhubuti tangu Siad Bare alipotolewa miaka 20 iliyopita.