Bali na sauti zao nzuri wanapoimba,kikosi hiki cha Bongo Flava ndicho kilichoindoa Bongo Movie kwa goli 2-0,Mchango wa timu zote mbili umeleta mafanikio makubwa sana kwa wahanga waliopatwa na matatizo ya mlipuko wa mabomu Gongolamboto wiki chache zilizopita.
 Hii ndio timu au kikosi cha Bongo Movie Kilichokubali matokeo pale kilipolazwa goli mbili bila.
 Wananchi walioingia uwanjani hapo sio tu kuburudisha nafsi zao,lengo kuu na madhumuni yao ilikuwa kuchangia wahanga wa mabomu ya Gongolamboto.Pongezi za dhati kwa kila mwananchi aliyeguswa na tukio hilo kwa wananchi wenzetu.
 Wasanii hao wakiingia uwanjani kuanza mtanange uliowaburudisha watu na kuleta mchango mkubwa kwa Taifa.Hongereni sana wasanii wa nyumbani kwa ubunifu wa hali ya juu na vipaji mlivyojaaliwa.
WASANII wa bongo fleva na wale wa filamu nchini kupitia mechi yao ya soka wamefanikiwa kukusanya na kukabidhi fedha pamoja na vyakula vyenye thamani ya Sh. milioni 76.7 kwa ajili ya kusaidia waathirika wa milipuko ya mabomu Gongo la mboto.

Akizungumza kwa niaba ya wasanii wenzake mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Dar es Salaam, msanii wa muziki huo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, alisema fedha hizo zilitokana juhudi za wasanii hao katika kuchangisha watu mbalimbali lakini pia mechi yao ya soka.
“Wasanii wote tuliguswa na tukio hili la wenzetu kupoteza maisha huku wengine wakihangaika kwa kukosa sehemu za kulala, kutokana na wengi wetu
kuwa na uwezo mdogo, ndipo tulipobuni njia za kupata fedha ili na sisi angalau tusaidie,” alisema Mwana FA.
Alisema kupitia mechi hiyo iliyochezwa baina ya wasanii wa muziki na filamu na wa muziki wakaibuka na ushindi wa mabao 2-0, wasanii hao waliweza kukusanya Sh milioni 43.2 na katika onesho lao la muziki na filamu waliahidiwa Sh milioni 11.5.

Alisema pia kupitia jitihada zao waliweza kupata na kukabidhi kutoka kwa wahisani magunia 200 ya sukari na mchele ambapo jumla ya fedha zote walizokusanya na vyakula ni Sh milioni 76.7.

Katika kukabidhi fedha hizo na vyakula, Mwana FA alikuwa ameongozana na baadhi ya wasanii wenzake ambao ni Jackline Wolper, Dude, Fid Q, Dataz wakiongozwa na Ruge Mutahaba wa Clouds FM.

Akizungumza mara baada ya kupokea fedha na vyakula hivyo, Waziri Pinda, alisifu jitihada na moyo wa kujituma wa wasanii hao na kuwezesha kupata kiasi hicho cha fedha.

“Kwa kweli sikutegemea kama wasanii hawa wangeweza kufanya jambo kubwa kama hili, nawashukuru sana kwani kupitia vipaji vyao wameweza kukusanya fedha nyingi ambazo zitasaidia sana ndugu zetu hawa, kwa kweli wamenigusa sana,” alisema Pinda.

Aliwataka watu wengine kuiga mfano kama huo na kujitolea kusaidia waathirika wa mabomu hayo kwa kuwa kwa sasa wanahitaji msaada wa kila aina kutokana na hali halisi waliyonayo.