Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu muugano wa majeshi ya nchi za magharibi yaanze kushambulia Libya, Kanali Gaddafi ametoa wito kwa waiislamu wamuunge mkono.
Gaddafi amewaambia wafuasi wake akiwa Bab al-Aziziya, kwenye kasri yake iliobomolewa na ndege za kivita hapo juma pili, kuwa harakati zinazoendelea dhidi yake ni vita dhidi ya waislamu.
Katika hotuba hiyo iliodumu kwa dakika tatu kwenye televisheni ya kitaifa, Kanali Gaddafi amesema kwa vyovyote vile jeshi lake litashinda na wala halitasalimu amri.
Wakati huo huo, shirika la NATO limepitisha azimio kuwa wanajeshi wake waanze kushika doria kwenye bahari ya Mediterranean ilikuzuia silaha na mamluki kuingia Libya.
Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron wanapendekeza kuwa NATO iongoze harakati hizo za kivita nchini Libya, lakini kiongozi wa Ufaransa Nicolas Sarkozy hajakubaliana nao.
Ufaransa ndio nchi ya kwanza kulitambua baraza la waasi wanaompinga Kanali Gaddafi.
Taarifa zinasema watu wengi wamekufa mjini Misrata, magharibi mwa Libya eneo ambalo limeshuhudia mapambano makali kati ya waasi na wanajeshi wanaomtii Kanali Gaddafi.
Kanali Muammar Gaddafi ametembelea kasri yake ilioharibiwa vibaya na makombora mapema wiki hii, ambapo ametabiri kuwa jeshi lake litawashinda waasi.