BAADA ya kutumia musuli wa fedha na kuweza kuonana na Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila wilayani Loliondo mkoani Arusha, na kuwaacha wanyonge wakisota, sasa vigogo hao huenda mambo yakawatumbukia nyongo.
Mchungaji Masapila ameapa kuwa vigogo waliofanya hivyo kwa kutumia njia za mkato na kufanikiwa kumwona na kunywa dawa, hawatapona magonjwa sugu yanayowakabili.

Mchungaji huyo mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema hali hiyo imesababishwa na kitendo chao cha kukiuka baadhi ya masharti ya tiba yake ambayo inakataza kufanyiwa biashara na wala kupewa upendeleo.

Hivi karibuni, baadhi ya maofisa wenye vyeo katika sekta mbalimbali nchini,
walidaiwa kutumia nafasi zao kushawishi askari wanaolinda usalama katika makazi ya Mchungaji Masapila, ili kuwavusha foleni na kupata tiba haraka.

Polisi walio eneo hilo kijijini Samunge, tarafa Sale, pia wamedaiwa kutumia nafasi zao kupitisha ndugu, jamaa na marafiki zao, jambo ambalo Mchungaji Masapila alionya kuwa halitawasaidia kwani dawa hiyo haifanyi kazi katika mazingira hayo.

"Huu ni uponyaji wa Mungu na Mungu huwa hatambui cheo au nafasi ya mtu, ukikosea utaratibu dawa inabaki kuwa maji ya kawaida," alifafanua Masapila.

Maelfu ya watu kutoka pande zote za nchi na nchi jirani wako katika kijiji hicho kwenye mbuga ya Sonjo, kata ya Digo-digo, Ngorongoro wakitumaini kupata tiba hiyo ya ajabu.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, alisema jana kuwa ofisi yake inafikiria kutenga siku maalumu na hasa Jumamosi, kwa watumishi wa umma na Serikali kwenda kupata tiba hiyo ili kupunguza msongamano na kuwawezesha kurudi mapema kwenye kazi zao za utumishi kwa Taifa.

Hata hivyo, haijulikani kama Mchungaji Masapila atakubaliana na wazo hilo, kwa maana alisisitiza kuwa mtoaji huyo wa dawa anazingatia kutokuwapo kwa upendeleo katika utoaji tiba hiyo.

Katikati ya wiki hii, vurugu zilidaiwa kuzuka karibu na eneo la tiba, baada ya watu wanaodhaniwa kuwa vigogo kulazimisha kuwapita wananchi wengine waliopanga foleni kwa ajili ya kupata tiba.

Hivi sasa watu wanalazimika kukesha kwa siku nne wakisubiri zamu ya kupewa dawa na Mchungaji Masapila ambaye sasa amepata usaidizi wa wachungaji wengine watatu wanaomsaidia kuchota dawa.

Hata hivyo, Masapila analazimika kugawa dawa hiyo kwa mkono wake mwenyewe, maana bila hivyo, tiba hiyo inayotokana na mizizi iliyochemshwa na maji, haitafanya kazi.

Mkazi wa Sonjo aliyevamia moja ya masufuria na kujichotea dawa na kuinywa Jumatatu alipata msukosuko mkubwa kwani tumbo lilipata maumivu makali na kulazimisha ‘Babu’ Masapila kuingilia kati kumsaidia.

Wakati hayo yakiendelea, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Akili Mpwapwa, alisema Jeshi bado halijapokea taarifa rasmi za vifo vinavyodaiwa kutokea katika mbuga ya Sonjo ambako maelfu wamepiga kambi wakisubiri tiba.

Hata hivyo Lali juzi alithibitisha vifo sita kati ya 14 vinavyodaiwa kutokea katika eneo la Samunge.

Lali alipozungumza jana na gazeti hili, alisema misururu ya watu wanaofuata matibabu imepungua na kubaki umbali wa kilometa 15 huku magari yakibaki kati ya 1,000 na 1,500 kutoka ya awali 3,000.

Alisema katika magari hayo yakiwamo malori na mabasi na magari madogo kila gari lina watu wasiopungua watano.

Kwa mujibu wa Lali, mtu mmoja alifariki dunia wakati akisubiri matibabu na alikutwa jana walipotembelea eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya alisema watu wamekuwa wabishi kwa kutoa wagonjwa hospitalini wakiwa mahututi na kuwaweka mistarini kwa ajili ya kupata dawa na hivyo kuzidiwa na kufariki dunia.

Mchungaji Masapila hutoa dawa hizo anazodai kuoteshwa na Mungu kwa Sh. 500 huku akidai kutibu magonjwa sugu yakiwamo ya Ukimwi, pumu, kisukari na mengineyo huku dozi yake ikiwa kikombe kimoja tu cha dawa hiyo.

Inadaiwa kuwa kutokana na misururu hiyo, gharama za magari zimeendelea kupanda kwani sasa wanaokwenda kwa magari ya kitalii wanalazimika kulipa kati ya Sh. 120,000 na Sh 150,000 na mabasi ni kati ya Sh 30,000 na Sh 50,000.