MWENYEKITI wa chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, amewaonya Watanzania wasiichezee amani iliyopo kwa kuwa ikitoweka, watajuta.
Akizungumza na umati wa vijana, Dar es Salaam jana, Mrema aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, alisema dalili zilizopo za kuvunjika amani, ziliwahi kutokea katika baadhi ya nchi ambazo sasa hazikaliki.

Katika mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Bakhresa Manzese, alisema dalili hizo, ikiwemo ya maandamano yanayodaiwa kuwa ya amani, ziliwahi kutokea katika nchi kama Madagascar na Somalia ambako sasa hakutawaliki.

Huku akishangiliwa na vijana hao katika mkutano huo wa amani uliokuwa na kaulimbiu: ‘Amani yetu bado tunaipenda’, Mrema alitoa mfano wa vurugu zilizotokea nchini Madagascar zikiongozwa na kiongozi wa upinzani, Andry Rajoelina ambazo zimeifanya nchi hiyo isitawalike.

Kwa mujibu wa Mrema, Rajoelina alitumia udhaifu na matatizo ya wananchi wakaanza maandamano kama yanayofanyika Tanzania wakafanikiwa kumtoa Rais wa nchi hiyo, Marc Ravalomanana madarakani lakini sasa kuna vurugu tupu.

Alisema matukio kama hayo pia yalifanyika Somalia ambako sasa ni zaidi ya miaka 10 hakuna serikali na kuongeza kuwa hata Zanzibar, CUF walianza hivyo hivyo kwa maandamano na matokeo yake watu wakafa na wengine kupata elemavu wa maisha.

Mrema alisema wakati watu wakiendelea kuishi na ulemavu huku wangine wakiwa wamepoteza ndugu zao huko Zanzibar, leo kiongozi wa upinzani, Maalim Seif Sharif anakula sahani moja na Rais Mohamed Shein.

Aliwashangaa wanaosema kuwa amenunuliwa na CCM kwa kutetea amani ya nchi na kufafanua kwamba tatizo lililopo mtu akitetea nchi yake na kupingana na baadhi ya fikra za watu, anaonekana kibaraka.

Alitamba kwamba yeye ni kiongozi wa upinzani aliyewahi kupata kura nyingi kuliko kiongozi yeyote wa upinzani nchini mwaka 1995, alipopata asilimia 28 ya kura zote na kuongeza kuwa, wakati akibezwa chuo kimoja cha Afrika Kusini, kimemtunukia Shahada ya Heshima ya Uzamivu (PHD).

Katika mkutano huo ulioandaliwa na Kamati ya Vijana Watanzania Wapenda Amani (KVT), Rais wa Vyuo Vikuu nchini, Mathias Kipala na Mwenyekiti wa chama cha Updp, Rajab Mrisho, walilaani maandamano ya chama cha Chadema na kuonya hali inaweza kuwa kama katika ajali za mabomu za Gongo la Mboto na Mbagala.