Mwendesha mashtaka wa Misri ametoa hati ya kumzuia Rais aliyeondoka Hosni Mubarak kusafiri pamoja na familia yake.
Msemaji wa ofisi ya mwendesha mashtaka alisema amri hiyo pia inapiga tanji fedha na mali zao.
Bw Mubarak aling'atuka Februari 11, baada ya kukaa madarakani kwa takriban miaka 30, kufuatia
kuibuka maandamano yaliyofanywa na umma ukimpinga.
Inaarifiwa kuwa afya yake ni duni, akiishi kwenye nyumba yake ya kifahari huko Sharm el-Sheikh, lakini hajaonekana wala kusikika hadharani tangu alipoachia madaraka.
Alikabidhi uongozi wake kwa jeshi, ambapo iliteua serikali ya mpito itakayoandaa katiba mpya na uchaguzi pia.
Shirika la habari Reuters limeripoti kuwa ofisi ya mwendesha mashtaka alisema kizuizi hicho cha kusafiri na kupiga tanji mali zake ilitolewa wakati malalamiko yalipotolewa- ambapo haijfafanuliwa- dhidi ya familia ya Bw Mubarak wanachunguzwa.
Misri tayari imeziomba serikali kadhaa kupiga tanji mali za familia ya Bw Mubarak nje ya nchi.
Waandamanaji pamoja na wanaopinga ufisadi wamekuwa wakishinikiza mali za familia ya Bw Mubarak zichunguzwe, ambayo inakadiriwa kuwa kati ya dola za kimarekani bilioni moja hadi bilioni 70.
Hata hivyo, mwakilishi wa kisheria wa Bw Mubarak amekanusha taarifa kuwa aliyekuwa Rais alijilimbikizia mali akiwa madarakani.