Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika shindano la kuchoma nyama litakalofanyika Jumamosi mkoani humo kwa kushirikisha baa tano zilizotinga fainali ya michuano hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Meneja wa Bia ya Safari ambao ndio wadhamini wakuu wa shindano hilo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Fimbo Butallah, alisema kuwa baa zilizofanikiwa kufika hatua ya fainali ni tano, ambazo ni Kalembo, 2000 Grocery, Mbeya Carnival, Sky Club na Nebana.
Butalla alisema kuwa maandalizi ya fainali hizo yamekamilika na bendi ya muziki wa dansi ya Tanzania One Theatre (TOT Plus) ndiyo itakayotoa burudani katika shindano hilo.
Alisema kuwa mshindi atajinyakulia kitita cha Sh.
Milioni Moja, mshindi wa pili Sh. 800,000, wa tatu Sh. 600,000, wa nne Sh. 400,000 na timu itakayoshika nafasi ya tano itaambulia Sh. 200,000.
"Kila kitu kinakwenda vizuri na kilichobakia ni siku hiyo ya fainali kufika, wote wamejiandaa kuonyesha ujuzi wao wa kuchoma nyama mbalimbali," aliongeza meneja huyo.
Mwaka jana mshindi wa shindano hilo jijini Dar es Salaam ilikuwa ni baa ya Kisuma iliyoko Temeke, mabingwa wa Arusha wakiwa ni Sakina na Mkulima iliibuka kidedea mkoani Kilimanjaro.