Spika wa Bunge, Anne Makinda, ametabiri kuwa mkutano ujao wa Bunge utakuwa moto kuliko uliopita na ameapa kwamba hatakipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM) kwani akifanya hivyo anaweza kusababisha machafuko nchini na kusababisha nchi isitawalike.
Aliyasema hayo jana mjini Bagamoyo wakati akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari baada ya kufungua semina ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na ofisi ya Bunge.
Kuhusu swali kwamba anaonekana kupendelea CCM, Makinda alisema hawezi kufanya hivyo kwa kuwa jambo hilo ni la hatari
na wananchi hawatakubaliana nalo kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha ghasia na nchi kutotawalika.
“Kwa dini yangu mimi naapa kabisa sitapendelea chama chochote cha siasa, ukipendelea chama fulani wananchi wanaona, vyombo vya habari vinaona na unaweza kusababisha nchi isitawalike kabisa,” alisema Makinda.
“Siwezi kukandamiza upinzani hata kidogo, hii nafasi ya Spika ni nafasi nyeti sana huwezi ukafanya mchezo huo maana amani itatoweka na kitakachofuata ni machafuko, na nimeapa sitapendelea kwa kuwa naogopa kuokota makopo barabarani,” alisema Makinda.
“Mimi natambua mamlaka na majukumu niliyopewa kikatiba, katika kuliongoza Bunge hivyo siwezi kujiingiza katika ushabiki na maamuzi ya aina yoyote ya upendeleo kwa sababu najua kwa kufanya hivyo naweza kuiingiza nchi katika machafuko makubwa,” alisema.
Akizungumzia malumbano ya wabunge, alisema hayo ni mambo ya kawaida katika mabunge yote duniani na wengine katika nchi mbalimbali wamekuwa wakifikia hatua ya hata kupigana.
Alisema wananchi hawana sababu ya kushangaa mijadala mikali iliyotokea kwenye Mkutano wa Pili uliopita kwa kuwa siku zijazo inaweza ikatokea mijadala mikali zaidi ya mkutano uliopita.
Alisema wabunge kuzomeana ama kutoka nje ya mkutano wa Bunge kwa kutoridhishwa na jambo fulani ni hali ya kawaida kwa kuwa wabunge hao hao wanaotoka nje baadaye hurudi bungeni na kuendelea na shughuli nyingine.
Wabunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walitoka nje ya ukumbi wa Bunge katika Mkutano wa Kwanza kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya kufungua Bunge la Kumi Novemba 18, 2010.
Wange hao walitoka tena nje ya ukumbi wa Bunge Februari 8, mwaka huu kupinga kupitishwa kwa marekebisho ya kanuni za Bunge ambazo tafsiri ya neno “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni” ilitolewa.
“Mbunge au wabunge kutoka nje ya ukumbi sio issue (suala) hata kidogo, jambo muhimu ni uamuzi wa Spika kuhusu jambo linlobishaniwa, mabunge mengine mambo yanayotokea mle yanatisha, tuliwahi kwenda Bunge la India tukashangaa kila mbunge anasimama anataka kuzungumza,” alisema Makinda na kuongeza:
“Kwa hiyo Bunge letu bado ni la kistaarabu kabisa, watu wasione ajabu yanayotokea mle.”
Kuhusu ushauri uliotolewa na mmoja wa waandishi wa habari kuwa afute kauli yake aliyoitoa bungeni kuwa wabunge wasome magazeti kama barua zingine za wasomaji, Makinda alisema hawezi kufuta kauli yake kwa kuwa alikuwa sahihi.
Alisema mwandishi aloiyeandika makala ya kumkosoa yeye na Bunge zima kuhusu utaratibu wa kutafsiri kambi rasmi ya upinzani alimkasirisha sana kwa kuwa hakujua ambacho alikuwa akikiandika.
“Sitaomba radhi na ambaye hataki kukubaliana na maoni yangu shauri yake, niliwaambia wabunge wasome magazeti kujifurahisha tu kwani baadhi ya mambo yanayoandikwa hayana ukweli wowote, mfano sisi tulichofanya ni kutafsiri kanuni kuhusu kambi rasmi ya upinzani bungeni, lakini yaliyoandikwa ni tofauti kwa kweli yale yalinikera sana mimi,” alisema.
Kuhusu kumnyima Mbunge wa Arusha Mjini, Chadema, Godbless Lema, kutoa ushahidi bungeni wa kauli yake kuwa Waziri Mkuu alilidanganya Bunge, Makinda alisema muda ulikuwa hautoshi.
Alisema baada ya Lema kumpelekea ushahidi wake kwa maandishi, alipeleka vielelezo hivyo kwa wataalamu na wanasheria wake ili wavifanyie kazi, lakini mpaka mkutano wa Bunge unamalizika hakukuwa na muda wa kujadili suala hilo.

LEMA AHOFIA MAAMUZI YA SPIKA
Wakati Makinda akisema hayo, Lema amesema ana wasiwasi wakirudi bungeni mwezi ujao Spika Makinda atazuia ushahidi wake dhidi ya kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutolewa mbele ya Bunge.
Lema alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, Spika Makinda atafanya hivyo kwa maelezo kwamba, suala hilo liko mahakamani.
Alisema awali katika Mkutano wa Bunge uliopita, Spika Makinda alijaribu kuzuia ushahidi huo, lakini hoja ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, kwamba kanuni ya Bunge inataka ushahidi utolewe mbele ya Bunge ndiyo iliyombana.
Lema alisema wasiwasi juu ya Spika Makinda kuzuia ushahidi wake kutolewa bungeni unakuja baada ya mahakama inayosikiliza kesi yao ya kuandamana bila kibali, mara ya mwisho kuonya kwamba, mambo yaliyo mahakamani yasiingiliwe na mihimili mingine ya dola.
Alisema pia kauli ya mawakili wa upande wa serikali waliyoitoa mahakamani kwamba, polisi wanafanya upelelezi wa kesi hiyo kwa siku 60 hadi 120, inamaanisha kwamba, hadi Mkutano wa Bunge wa Aprili unaisha, polisi watakuwa bado hawajakamilisha upelelezi huo, hivyo nafasi ya ushahidi wake kutolewa mbele ya Bunge haitapatikana.
“Lakini mimi msimamo wangu uko palepale kuhusu kauli ya Waziri Mkuu aliyoitoa bungeni.
Wakiruhusu niwasilishe ushahidi wangu bungeni, atapaswa ajiuzulu, kwani ikiwa polisi hawajakamilisha upelelezi, ni mashineri (mfumo) gani iliyomuarifu kusema kuwa matukio ya Arusha yalichochewa na Chadema?” alihoji Lema.