Agizo la Serikali la kuwataka wafanyabiashara ya sukari kutouza kilo moja kwa zaidi ya Sh. 1700 limegonga mwamba ambapo hadi sasa bado bidhaa hiyo inauzwa kati ya Sh. 1800 hadi Sh. 2000 kutegemea na eneo jijini Dar Salaam.
Uchunguzi uliofanywa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam umebaini kuwa agizo hilo la serikali ambalo lilitolewa na Rais Jakaya Kikwete limepuuzwa na wafanyabiashara hao.
Wafanyabiashara hao walisema kinachowafanya wauze kwa bei ya zaidi ya Sh. 1,700 ni kutokana na wao kununua mfuko mmoja wa kilo 50 kwa kati ya Sh. 84,000 hadi Sh. 90,000.
Kauli ya serikali imeonekana kuzua mkanganyiko kwa kuwa wafanyabiashara wanadai kwamba endapo wakiuza kwa bei ilipendekezwa na serikali hawatapata faida.
Uchunguzi huo uliofanywa katika maeneo ya Mbezi Beach, Mwenge, Sinza na Makongo ulibaini kuwa sukari inauzwa kwa bei ambayo inapingana na aliyosema Rais Kikwete.
Hivi karibuni bei ya sukari imekuwa ikipanda siku hadi siku huku juhudi za serikali za kutaka ishuke zikigonga mwamba.
Serikali iliwaagiza wafanyabishara kushusha bei huku ikishindwa kuviagiza viwanda na wasambazaji wakubwa kutouza kwa bei ya juu.