Mkurugenzi wa bendi ya Talent, Husseni Jumbe, amewataka mashabiki wa bendi ya Mlimani Park 'Sikinde' kutomuona Shaaban Dede kama msaliti kwa uamuzi wake wa kuhamia kwa wapinzani wao, Msondo Ngoma 'Baba ya Muziki'.(Pichani ni Shaaban Dede).
Jumbe aliyewahi kuzifanyia kazi bendi hizo mbili kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki aliiambia Sikinde ilipokuwa ikichuana na Msondo, alisema kuhama kwa Dede iwe changamoto kwa Sikinde, ambayo inapaswa ijipange ili kusimama imara.
Mtunzi na muimbaji huyo nyota nchini alisema haoni kosa kwa Dede kuhamia Msondo iwapo kama ameamua mwenyewe kurejea nyumbani.

"Binadamu yeyote huwa na baba na mama, Dede amerejea kwa baba yake, sioni kama anastahili kubebeshwa lawama za kuonekana ni msaliti, Sikinde wakijipanga wanaweza kusimama imara bila mkongwe huyo," alisema Jumbe.
Aliongeza, Dede sio mwanamuziki wa kwanza kuhama na hivyo asisakamwe kwa sababu muziki ni kazi na mwenyewe huenda kaona Msondo kuna masilahi kuliko alipokuwepo.
Shaaban Dede maarufu kama 'Kamchape' au 'Super Motisha', ambaye kwa sasa anataka afahamike kama "Mzee wa Loliondo', aliihama Sikinde wiki iliyopita ikiwa ni baada ya kuitumikia kwa miaka 21 na kutua katika bendi yake ya zamani ya Msondo.