Kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch HRW, kitengo maalum cha polisi cha Uganda kimefanya utesaji, kutumia nguvu kupita kiasi na mauaji holela.

Ripoti hiyo imesema maafisa wa kikosi maalum cha polisi huwapiga watu mara kwa mara na vifaa kama marungu, chupa na vyuma.
Imesema katika matukio mengine walikuwa wakiwaingizia pini chini ya kucha za washukiwa.
Msemaji wa polisi wa Uganda alisema kumekuwa na ripoti za utesaji, lakini idadi yao imepungua.
Ripoti hiyo yenye kurasa 59 imetolewa kutokana na ushahidi wa zaidi ya watu 100 na waliokuwa washukiwa, familia zao, na waliokuwa kwenye kikosi cha polisi pamoja na ambao bado wapo kwenye nafasi hizo.

'Magari yasiyo na nembo'

Imeonyesha madai ya kuwepo mauaji holela ya watu sita mwaka 2010. Watu wawili walikufa kutokana na kupigwa wakati wa kusailiwa, huku wengine wanne wakipigwa risasi na kufa walipokamatwa, HRW ilisema.
Kitengo hicho maalum cha polisi hukamata watu wanaodaiwa kufanya uhalifu wa makosa mbalimbali, yakiwemo makosa madogo na ugaidi.
Ripoti hiyo inaeleza, " Wafanyakazi wa kitengo hicho hufanya shughuli zao kwenye magari yasiyo na nembo ya polisi, huvaa nguo za kiraia yasiyo na alama za vyeo vyao, na kubeba bunduki mbalimbali, zikiwemo bastola na bunduki kubwa."
Ilisema kuwa kitengo hicho kimemteua mkurugenzi mpya mwaka jana, iliyoanzisha huduma ya simu ya bure na idaraya kutoa malalamiko.
Msemaji wa polisi wa Uganda Judith Nabakooba alisema: " Kesi zinapoletwa kwetu hufanyiwa uchunguzi na hatua huchukuliwa."
Rais Yoweri Museveni aliunda kitengo hicho mwaka 2002. Mwanzo kikiitwa Operation Wembley, kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa Violent Crime Crack Unit na baadae Rapid Respone Unit.