WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amemwagiza Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli kusitisha kwa
muda zoezi la bomoa bomoa za nyumba na majengo yaliyojengwa kwenye hifadhi ya barabara hadi hapo tathmini ya nchi nzima itakapofanywa. Akizungumza na wananchi wa Chato kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya shule ya msingi Chato mjini hapa, Waziri Pinda alisema zoezi hilo ni zuri kwa kuwa linatekeleza sheria za nchi lakini kasi yake ni kubwa mno.

“Kwanza nawashukuru wananchi wa Chato kwa kumchagua Dk.Magufuli, huyu ni jembe
muhimu la wananchi na hata serikali, ila namuomba asitishe kwanza zoezi la ubomoaji”, alisema Waziri Pinda.

Alisema ni vyema zoezi hilo Waziri Magufuli akalisimamisha kwa muda, ili tathmini ifanywe nchi nzima kubaini majengo na nyumba zitakazobomolewa na kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi.

Waziri Pinda ambaye pamoja na kutoa agizo hilo, alisema Waziri Magufuli amefanya kazi
kubwa ndio maana wamempatia wizara ya ujenzi ili kuhakikisha anaisimamia kikamilifu.

“Kazi kubwa aliyonayo sasa ni kusimamia makandarasi ili wafanye kazi zao kwa viwango
vinavyotakiwa na kwa muda uliopangwa”, alisema Waziri Pinda.

Aliongeza, kwa muda mrefu sekta ya barabara imekuwa ikidorora na hivyo rais hakukosea kumteua Dk. Magufuli kusimamia sekta hiyo.

“Hapa ataweka mambo sawa na wananchi watanufaika na miundombinu ya barabara”,alisema Waziri Pinda.

Bomoa bomoa hiyo ilianza nchini mwanzoni mwa mwaka huu ambapo Waziri Magufuli aliwataka Wakala wa barabara nchini Tanroads, kubomoa majengo yote yaliyojengwa kwenye hifadhi ya barabara.