Rais Jakaya Kikwete akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa tano wa Kimataifa wa Tasnia ya Uzinduaji (EITI) mjini Paris, Ufaransa, uliozungumzia matarajio ya baadaye ya tasnia hiyo na uwazi katika masuala ya fedha. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, Sri Mulyani Indrawati, Mwenyekiti mtarajiwa wa EITI, Clare Short, na Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza.Raisi nini aliongea kwenye mkutano huo?
KUNA uwazi na uwajibikaji zaidi na urahisi sasa katika kujua ni kiasi gani cha kodi kimekusanywa kutokana na sekta ya madini nchini kuliko ilivyokuwa awali.

Hayo yalisemwa jana na Rais Jakaya Kikwete alipozungumza katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Tasnia ya Uziduaji (EITI) jijini Paris, Ufaransa kwa mujibu wa hotuba yake iliyopatikana Dar es Salaam.

Alisema awali kampuni za madini ndizo zilikuwa zikitoa taarifa za kodi na mrabaha kiasi gani unaopatikana na Serikali kutegemea uaminifu wa kampuni hizo.

Lakini sasa Serikali imeanzisha chombo cha kukagua mahesabu katika tasnia ya madini ambayo hutoa taarifa na kuzifanyia uhakiki juu ya uendeshaji wa kampuni za madini nchini.

“Awali kulikuwa na hatari ya kampuni kutosema ukweli na hivyo raslimali zetu kuvunwa bila kampuni hizo kulipia kodi … kulikuwa na hofu ya kweli kuwa tungeweza kupoteza madini yetu kwa wawekezaji na kupata kitu kidogo au kutoka kapa,” alisema Rais.

Alisema kwa kuwa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini hivi sasa, Watanzania wanaweza kusema kwa kujiamini kwamba mambo yameanza kubadilika na yataendelea kubadilika na kuwa bora zaidi.

Aliongeza kuwa Tanzania inajivuna kuwa mwanachama wa EITI ambayo unaendana vema na juhudi za Serikali katika kudhibiti shughuli za uchimbaji madini.

“EITI imetuhamasisha sana na imeimarisha usimamizi wetu na suala la uwajibikaji na uwazi katika mapato kwenye uvunaji wa raslimali zetu. Ingawa EITI ni dhana mpya nchini, lakini imeanza kuonesha matokeo mazuri. Imetuvusha hatua moja mbele,” alisema.

Mwezi jana, Tanzania kwa mujibu wa Rais, ilichapisha ripoti yake ya kwanza ya EITI ikielezea malipo yaliyofanywa na kampuni za madini serikalini kuanzia Julai mosi 2008 hadi Juni 30 mwaka jana.

“Ripoti hiyo inasaidia kuwafahamisha Watanzania juu ya mapato yanayotokana na tasnia ya uchimbaji. Pia utoaji wa ripoti hiyo, umeibua mijadala kwa umma na bungeni juu ya dhima ya Serikali katika ukusanyaji wa kodi na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wetu,” aliongeza.

Alisema masuala kadhaa yaliibuliwa na ripoti hiyo ambayo Serikali hivi sasa inafuatilia ili kuyatatua. Mathalan alisema Serikali imempa kazi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya kuangalia upungufu wowote uliojitokeza katika malipo kati ya kampuni za madini na wakala wa Serikali.

Rais alisema Tanzania inajivunia kuwa sehemu ya familia ya EITI duniani na kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza kanuni za EITI. “Tunakubaliana na mchakato wa EITI, kwa sababu unakwenda sawia na sera yetu ya kukuza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa matumizi ya raslimali zetu,” alisema.

Aliongeza kuwa mchakato huo ni muhimu katika kuleta maendeleo endelevu na kutokomeza umasikini nchini.