RAIS Jakaya Kikwete ameagiza chakula cha akiba kiingizwe katika masoko ya mijini na hasa Dar es Salaam mara moja, ili bei ya mahindi ipungue na kupunguza makali na gharama ya maisha kwa wananchi.
Rais Kikwete ameagiza kuwa kazi hiyo ya kuingilia soko na kupunguza bei ya chakula kwa wananchi, iwe ya nyongeza na ya kudumu ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wakala wa Akiba ya Chakula ya Taifa (NFRA). Uamuzi huo wa Rais, utasaidia pia kupungua kwa mfumuko wa bei ambao mara nyingi kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) za kila mwezi, umekuwa ukichangiwa kwa kiwango kikubwa na ongezeko la bei za chakula na petroli.

Rais amesema miji ya Tanzania ina masikini wengi na kuwa gharama kubwa ya masikini hao ni bei kubwa ya chakula na ni wajibu wa Serikali kuchukua hatua za makusudi kuwapunguzia wananchi gharama hizo za maisha kwa kuingiza chakula cha bei nafuu katika masoko.

Rais Kikwete ametoa maagizo hayo alipotembelea maghala ya NFRA mjini Dar es Salaam kama mwendelezo wa ziara zake na wizara na taasisi zao.

Alisema kama hatua za kuingilia soko zingechukuliwa tangu Oktoba mwaka jana wakati bei ya mahindi ikiwa Sh 300 kwa kilo Dar es Salaam, bei hiyo isingepanda hadi Sh 430 za sasa.

“Hii ndiyo kazi yetu kuanzia sasa, yaani kuhakikisha tunaingilia soko, kuingiza chakula cha kutosha na hasa mahindi, kwa sababu hiki ndicho chakula kikuu cha Watanzania na kuhakikisha kuwa tunashusha bei hiyo ya mahindi hadi Sh 300 katika kipindi kifupi iwezekanavyo,” Rais aliwambia maofisa wa wizara na wakala huo.

Alisema lazima viongozi waelewe kuwa hata mijini kuna upungufu wa chakula. “Tafsiri ya njaa ni kama mji haupati chakula cha kutosha basi kuna njaa. Hivyo tujipe mamlaka ya kuingiza haraka sokoni ili kulinda wananchi, kwa sababu hatuwezi kuwaacha mikononi mwa wafanyabiashara binafsi wa chakula ambacho kichocheo chao kikubwa ni faida,” alisema Rais na kuongeza:

“Hii sasa ni kazi yetu ya kila siku, yaani kufuatilia masoko na kuhakikisha kuwa kinakuwapo chakula cha kutosha ili kupunguza bei. Chezeni na soko la Dar es Salaam ili kuhakikisha kuwa bei zinakwenda chini haraka iwezekanavyo.

“Twendeni katika masoko yote; Tandale, Tandika na kwingineko, si kujua bei ya chakula lakini kujua pia ni kiasi gani cha chakula kinahitajika ili kushusha bei kwa ajili ya wananchi.”

Alisema si busara kwa mahindi kubaki maghalani kusubiri njaa wakati bei za vyakula zinapanda kwa kasi.

“Nyie mna wajibu wa kulilisha Taifa hili. Tuhakikishe tunaifanya kazi hii vizuri. Kazi ya kulisha Watanzania haiwezi kuachiwa wafanyabiashara binafsi. Ni kweli Serikali haitaingia katika biashara ya chakula, lakini tunao wajibu wa kupunguza bei na makali ya maisha kwa wananchi,” alisema Rais.

Hivi karibuni akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema hali ya chakula si mbaya na kuwataka Watanzania kokote waliko wakiona dalili za upungufu wa chakula watoe taarifa ili wasaidiwe.