Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema kundi lenye maskini wameongezeka kwa kasi zaidi nchini ni la vijana wanaohama toka vijijini kwenda kuishi mijini kwa sababu ukuaji wa miji unaendelea kwa kasi kubwa kupita uwezo wa shughuli za uchumi kutengeneza ajira mpya.
Akifungua mkutano wa 16 wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti kuhusu kuondoa Umaskini (Repoa) jijini Dar es Salaam jana, alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo kunahitajika kuweka vivutio vitakavyoongeza vipato katika kilimo, viwanda vidogo vidogo na ajira za kujitegemea.
Pinda alisema kama asilimia 80 ya Watanzania wanategemea kilimo kwa maisha yao na sehemu kubwa ya maskini wapo katika kundi hilo ni dhahiri kwamba kunahitajika kuweka nguvu zaidi katika eneo hilo.
Ni muhimu kuhimiza ujenzi wa viwanda vinavyoongeza thamani ya raslimali na kusindika mazao, vyote vikilenga kuzalisha ajira zaidi. Kupungua kwa umaskini kutaendelea kutegemea kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kutumia fursa nyingi tulizo nazo katika nyanja mbalimbali,” alisema.
Waziri Mkuu alisema serikali inaandaa mpango kabambe wa kuwawezesha wasomi kujiajiri katika shughuli mbalimbali za kiuchimi ili kukabili tatizo la ajira nchini. 
Mpango huo umelenga kuwawezesha vijana wasomi walio tayari kujituma kujiajiri katika fani za kilimo, ufugaji, uvuvi, ujenzi, ufundi na maeneo mengineyo na kuiomba Repoa kusaidia jitihada hizo za serikali katika kutafiti namna bora ya kutekeleza azma hiyo.
Alisema taarifa zinaonyesha kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kutopungua kwa umaskini wa wananchi wengi ni pamoja na kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu ambalo haliendani na kiwango cha ukuaji wa uchumi.
Kwa sasa kiwango cha ukuaji wa uchumi ni wastani wa asilimia sita wakati kiwango cha ongezeko la idadi ya watu nchini kinakadiriwa kufikia asilimia tatu.
Pinda alisema taasisi za tafiti hazijaleta matumaini makubwa hususan upande wa uchumi na kuzitaka kujielekeza katika tafiti ambazo zitachangia kuboresha uchumi na kukabili changamoto zinazoikabili serikali na wananchi kwa ujumla katika kuondoa umaskini na kuboresha maisha yao.
Mkutano huo wa Repoa ambao unamalizika leo unawakutanisha wasomi, watafiti na wadau mbalimbali unachambua kiini cha umaskini na kupendekeza  njia zinazofaa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kupiga vita umaskini.(Maelezo zaidi nenda Nipashe)