Pamoja na kwamba ratiba ya vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, vinavyoanza jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili kuanzia Machi 22, ikionyesha havitajadili muswada wa Sheria ya Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, amesema muswada huo utawasilishwa bungeni kama ilivyopangwa.
Juzi, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa, Jossey Mwakasyuka, alitoa ratiba ya vikao vya kamati akieleza kwamba miswada kadhaa itawasilishwa kwenye kamati na kujadiliwa ukiwemo ule wa famasia wa 2010.
Alitaja miswada mingine kuwa ni wa marekebisho ya sheria ya ukanda wa uchumi, manunuzi ya umma na ule wa marekebisho ya sheria mbalimbali.
Lakini Jaji Werema alisema jana kwamba muswada huo utawasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na kwamba kabla haujawasilishwa wananchi watapata fursa ya kutoa maoni yao (public hearing).
“Sasa hivi sipo kwenye nafasi nzuri ya kuzungumzia hilo, lakini nina uhakika kwamba utakwenda na utapita kwenye kamati ili wananchi waweze kutoa maoni yao...nitafute wiki ijayo nitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa taarifa za uhakika zaidi,” alisema.
Akiahirisha Mkutano wa Pili wa Bunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliahidi kwamba serikali ingewasilisha bungeni muswada wa kuruhusu bunge liunde tume ya kuratibu maoni ya
katiba mpya katika mkutano wa bunge wa Aprili mwaka huu.
Pinda aliahidi kuwa tume hiyo itakapoundwa itapewa maelekezo ya jinsi itakavyofanya kazi na kwamba bunge litatoa maelekezo ya namna ya kufanikisha utekelezaji huo.

Watu bwanaa wanadai KATIBA MPYA NI LAZIMA,ukiwauliza ya zamani ina nini na mpya iwe na nini hawana jibu....kazi kwelikweli.