Viongozi wa kitaifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wameondoka nchini kwenda Liberia, kuhudhuria mkutano wa vyama vya kidemokrasia Afrika.
viongozi hao ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ambaye pia kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na Katibu Mkuu Dk. Wilibrod Slaa

Mkutano huo wa siku mbili unaanza leo na utahudhuriwa na viongozi wa vyama toka nchi mbalimbali za Afrika ambazo ni wanachama wa umoja huo.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mnyika, ilieleza kuwa Mbowe na Dk. Slaa watapata pia fursa ya kukutana na Rais Ellen Johnson Sirleff wa Liberia ambaye ni Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika.
Mkutano huo utaongozwa na Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika Dk. Kizza Besigye, ambaye pia ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha FDC cha nchini Uganda.
Pamoja na ajenda nyingine, mkutano huo pia utajadili hali ya kisiasa ya Afrika ya Kaskazini na mabadiliko ya msingi ya kimfumo katika uendeshaji wa uchaguzi barani Afrika.
Aidha kupitia mkutano huo vyama shiriki vitabadilishana uzoefu kuhusu demokrasia na kuleta maendeleo katika maeneo yanayoongozwa na vyama wanachama wa umoja huo.