RAIS Jakaya Kikwete ameiagiza Wizara ya Uchukuzi kuongeza kasi ya kuvunja mkataba baina ya Serikali na Kampuni ya Rites Consortium ya India uliounda Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ili hatua nyingine za utendaji ziendelee.
Aidha, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imemlalamikia Rais kuwa inapata shida kudhibiti makosa ya vyombo vya usafiri hasa vya nchi kavu kwa kuwa baadhi ya maofisa wa Polisi wanavimiliki hivyo wanashindwa kuvikamata na hata wakifanya hivyo, vinaachiwa.

Akizungumza na watumishi wa Wizara ya Uchukuzi, Dar es Salaam ikiwa ni mfululizo wa ziara zake kutembelea wizara mbalimbali, Rais Kikwete amesema, amefarijika na utendaji kazi wa wizara hiyo, lakini bado kasi zaidi inahitajika ikiwa ni pamoja na ya kusitisha mkataba wa Rites.

“Nimefarijika na utendaji wenu, ziara hii inalenga kujifunza na kuona yale tulioelezana awali kama mmeyafanyia kazi kwa kiasi gani, lengo ni kuwatumikia Watanzania….hili la Rites kasi ya kuachana nao muiongeze…iongezeke,” amesema Rais Kikwete leo.

Serikali iliingia mkataba Rites mwaka 2006 ambao ulisababisha kuvunjwa kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kuunda TRL ambapo mbia huyo ana asilimia 51 huku Serikali ikiwa na uwekezaji wa asilimia 49.

Mgogoro wa kutaka kuvunjwa kwa mkataba huo wa miaka 25, uliibuliwa na wafanyakazi wa TRL na kushika kasi mwishoni mwa mwaka 2009 baada ya Rites kushindwa kuwalipa wafanyakazi mishahara, lakini juhudi kadhaa zilichukuliwa na Serikali hadi hivi sasa inaposubiriwa kuvunjwa rasmi mkataba huo.

Rais aliitaka wizara hiyo kuhakikisha kuwa inakomesha na kumaliza kero zinazochangia kuwepo kwa migomo na migogoro ya mara kwa mara baina ya wafanyakazi wa reli na menejimenti zao kama ilivyokuwa TRL na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kwa kuwa hali hiyo inarudisha nyuma ufanisi.

Alisema, hataki kusikia tena hadithi ya migomo kwa kuwa sasa imekwisha na kuitaka Wizara kuangalia namna viongozi katika ngazi ya menejimenti wanavyochaguliwa kwani wengi wao wanakuwa ni makada wa vyama badala ya watendaji wenye ujuzi katika utawala na biashara.

Akijibu hotuba ya Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu kuhusu tatizo la kimfumo linavyochangia mgogoro wa kiutendaji Tazara, Rais alisema, “Tatizo sidhani kuwa ni mfumo, unaweza kuwa na mfumo mzuri lakini watu wabaya, sisi ndiyo tuna shida, badala ya kuchagua wenye uwezo, tunachagua makada.”

Alisisitiza wizara ifikirie kwa makini suala la kuwaachisha kazi wafanyakazi wa Reli na kisha watu hao hao wanataka kuajiriwa tena na kutaka kitu cha kwanza kuwa maslahi ya Taifa mbele.

Kuhusu Sumatra, awali Rais alihoji inapandishaje nauli, na alipewa mchanganuo na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Israel Sekirasa kuwa mamlaka ya kupanga nauli imepewa ngazi za mikoa, lakini alidai kuna mgongano wa kimaslahi unaotokana na baadhi ya maofisa wa polisi kumiliki daladala na magari ya abiria.

“Kuna shida kubwa Mheshimiwa Rais, baadhi ya maofisa wa polisi ndiyo wamiliki wa vyombo vya usafiri vya abiria, hivyo hata vikikosea havikamatwi na ikitokea, vinaachiwa bila hatua yoyote,” alidai Sekirasa.

Kwa upande wake, Rais alicheka na kusema, “Ya leo kali” maneno yaliyosababisha hadhira yote kuangua kicheko.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliitaka wizara iharakishe ujenzi wa Reli ya Kati na kubainisha namna ambavyo Serikali itahusika katika ujenzi kama ni kushirikiana na wawekezaji, kukopeshwa au sekta binafsi kujenga na kushirikiana kiuendesha.

Masuala mengine ambayo Rais aliitaka wizara kuyafanyia kazi baada ya hotuba ya Nundu, ni pamoja na kuboresha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), kuondoa msongamano bandarini kwa mizigo kutokaa zaidi ya siku tano.

Nundu katika hotuba yake pamoja na mambo mengine, alisema wana mpango wa kuanza kutumia treni kusafirisha abiria katika Jiji la Dar es Salaam katika kipindi cha miezi saba ijayo ikiwa zitapatikana Sh bilioni 4.7.