Ndege iliyokuwa imewachukua wafanyakazi wa ndani 86 kutoka Madagascar, ambao walisema walikuwa wakinyanyaswa Lebanon, imewasili kwenye mji mkuu, Antananarivo.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, serikali ya Madagascar ilituma ndege kufuatia vifo vya wafanyakazi wa ndani 17 mwaka uliopita.
Leonie, mwenye umri wa miaka 25 alisema, "Mwajiri wangu alikuwa akinipiga na hakunilipa mshahara wangu. Nina furaha sana kurudi nyumbani."

Takriban raia 7,000 wa Madagascar wanasadikiwa kufanya kazi Lebanon.
Waziri mkuu Camille Vital alisema, "Kumekuwa na vifo vingi."
Wizara inayoshughulikia idadi ya watu ilisema ilipokea maombi kutoka kwa wafanyakazi wa nyumbani 600 ya kurejea nyumbani ambao waliwakimbia waajiri wao.
Mwaka 2009, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilitoa wito kwa serikali ya Lebanon kuchunguza vifo vya wafanyakazi wa nyumbani wa kigeni wanaofanya kazi nchini humo.
Shirika hilo lilisema, mwaka jana mfanyakazi mmoja wa kigeni alikuwa akifariki dunia kila wiki.