Yanga inayopigana kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jana usiku ilielekea mjini Bagamoyo mkoani Pwani kwa lengo la kujiandaa na mechi yake ya Jumamosi dhidi ya mahasimu wao, Simba iliyoko Zanzibar.
Licha ya viongozi wake kuficha mahali ambako timu hiyo inaenda kuweka kambi, Wana-Jangwani hao waliorejea
jijini Dar es Salaam juzi usiku wakitokea Morogoro ilikokuwa inavaana na Ruvu Shooting, walikwenda Bagamoyo jana na leo wanatarajia kuanza mazoezi makali ili kupata stamina.
Kocha wa timu hiyo, Mganda, Sam Timbe, alisema kuwa anaenda kuwapa wachezaji wake mbinu za kuimaliza Simba aliyoiona mara tatu tangu awasili nchini.
Timbe alisema kuwa hana rekodi ya kuogopa wapinzani na hivyo anaahidi kwamba ushindi utapatikana ili waweze kumaliza wakiwa juu msimu huu.
"Ninajua kuna timu nne ambazo zinaweza kuchukua ubingwa, kwa hiyo tutafanya bidii ili kujiweka katika nafasi nzuri," alisema kocha huyo ambaye ana rekodi ya kuzipa mafanikio timu mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Timbe alisema kuwa wachezaji wa Yanga wameanza kumuonyesha kile anachokihitaji na malengo ya kumaliza wakiwa mabingwa yanaweza kupatikana.
Afisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, aliliambia gazeti hili kuwa wachezaji wote wataingia kambini jana usiku bila ya kutaja wanakokwenda.
"Leo (jana) usiku ndio vijana wataingia kambini, ni msituni, hatuwezi kutaja," alisema kwa kifupi.
Aliongeza kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri isipokuwa kiungo, Nurdin Bakari, ambaye anakabiliwa na uchovu baada ya kufanya mazoezi ya nguvu hivi karibuni.
Katika mchezo wa juzi kiungo huyo tegemeo aliyejiunga Jangwani akitokea Simba hakucheza na hakuwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba pamoja na kipa Mserbia, Ivan Knezevic.
Yanga inaongoza ligi na ikifanikiwa kuifunga Simba itakuwa imejiweka kwenye mazingira mazuri ya kuwavua watani zao ubingwa na kumaliza machungu ya kutupwa nje katika mashindano ya Kombe la Shirikisho na Dedebit ya Ethiopia mwezi uliopita.
Hata hivyo, Yanga imeizidi Simba mchezo mmoja huku Azam FC waliopania kumaliza katika nafasi mbili za juu msimu huu ikiwa imewazidi mabingwa hao watetezi mechi mbili.