Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete leo, Jumanne, Machi 15, 2011, ametembelea Wizara ya Fedha
(Hazina), ikiwa ni mwanzo wa ziara za kutembelea Wizara mbalimbali
kujionea utendaji wa Serikali, kuangalia utekelezaji wa maagizo ya
Serikali na yale aliyoyatoa alipotembelea wizara zote mwanzoni mwa
mwaka 2006, mwezi mmoja tu baada ya kuwa ameingia madarakani.

Aidha, Rais baada ya kuwa ametembelea Wizara ya Fedha ametembelea
Kitengo cha Long Room cha Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA).

Katika mazungumzo na viongozi wa Wizara na taasisi zote zilizoko chini
ya Wizara hiyo, Rais Kikwete ameelezea majukumu matatu makuu ya Wizara
hiyo kama ifuatavyo:

(a) Kusimamia Kukua kwa Uchumi

Rais Kikwete amesema kuwa wajibu kipaumbele katika miaka mitano ijayo
iwe ni kwa Wizara ya Fedha kusimamia na kutafuta njia za kuleta
utulivu zaidi katika uchumi kwa kubuni mikakati bora zaidi ya
kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi zaidi na hivyo
kupunguza umasikini kwa haraka zaidi. Hivyo, Rais amesema kuwa hata
Bajeti ya Serikali ni lazima ilenge katika sekta zitakazoharakisha
zaidi kasi ya kukua kwa uchumi.

Sambamba na agizo hilo, Rais Kikwete pia ameielekeza Wizara ya Fedha
kutafuta njia za haraka na bora zaidi za kupunguza mfumuko wa bei ili
kuwapatia wananchi unafuu zaidi wa maisha.

(b) Ukusanyaji Mapato ya Serikali

Rais Kikwete amesisitiza kuwa Hazina ndiyo moyo na roho ya Serikali na
kwamba Wizara hiyo isipofanya kazi ya kukusanya mapato ni dhahiri
shughuli za Serikali zitaathirika.

Rais amewasifu watumishi wa Wizara ya Fedha kwa kufanya vizuri katika
ukusanyaji wa mapato ya Serikali lakini akawataka waongeze juhudi
zaidi na wafanye vizuri zaidi. Ameambiwa kuwa mapato ya Serikali
yameongezeka kutoka makusanyo ya kiasi cha shilingi bilioni 215 kwa
mwezi mwaka 2005 wakati Rais kikwete anaingia maradakani hadi kufikia
wastani wa shilingi bilioni 420 kwa mwezi kwa sasa.

(C) Kusimamia Matumizi ya Fedha ya Serikali

Rais Kikwete amesema kuwa jukumu la tatu la msingi la Wizara hiyo ni
kusimamia matumizi ya fedha zinazokusanywa akiwakumbusha viongozi hao
kuwa fedha za Serikali siyo shamba la bibi na wala makusanyo hayo ya
kodi siyo sawa na ubani wa kilioni.

Amesema kuwa fedha za Serikali baada ya kukusanywa ni lazima zitumike
vizuri na kwa shabaha zilizokukusudiwa na akaelezea ni sababu hiyo
iliyopelekea Serikali kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi wa
matumizi ikiwa ni pamoja na kuunda nafasi ya Naibu Mhasibu Mkuu wa
Serikali kwa ajili ya kusimamia fedha zinazopelekwa kwenye Halmashauri
mbalimbali nchini na pia kuanzisha nafasi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali.

(D) Maagizo Mengine Makubwa

       (i) Rais Kikwete amesema kuwa moja ya maeneo ambayo bado yana
matatizo katika Wizara hiyo ni shughuli ya Manunuzi na ameitaka Wizara
ya Fedha kuhakikisha kuwa wanaajiriwa watu wenye ujuzi na elimu ya
masuala ya ununuzi lakini ambao pia ni waaminifu.

       (ii) Rais Kikwete pia ameitaka Wizara hiyo kukabiliana na
tatizo la kucheleweshwa kulipwa kwa mishahara mipya hasa ile ya
watumishi wapya katika Serikali. Aidha, amerudia maelekezo yake kuwa
Halmashauri nchini haziwezi kuruhusiwa kuhamishahamisha watumishi bila
na kuwa na fedha za kulipia uhamisho huo.

       (iii) Kuhusu malipo ya mishahara na marupurupu mengine ya
watumishi, Rais Kikwete ametaka umakini mkubwa katika kuhakikisha kuwa
haki za watumishi zinalindwa na watu hao kulipwa malipo yao ya haki na
kwa wakati.

       (iv) Kuhusu malipo ya wasataafu wa iliyokuwa Jumuia ya Afrika
Mashariki iliyovunjika, Rais Kikwete ametaka wote wanaostahili kulipwa
mafao yao na hawajalipwa hadi sasa walipwe, hata kama ni kweli kuwa
wengi wa watumishi hao tayari wamelipwa.

       (v) Kuhusu mikopo kwa watumishi wa Serikali, Rais Kikwete
amesema amefurahishwa na kwamba Wizara ya Fedha inakamilisha taratibu
za kuwakopesha watumishi hao, kama wanavyokopeshwa Wabunge. Aidha,
ameongeza kuwa Wizara iangalie uwezekano wa hata kuwadhamini watumishi
hao ili waweze kukopa moja kwa moja kwenye taasisi za fedha nchini.

       (vi) Kuhusu Deni la Taifa, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo
la heri sana kuwa Tanzania sasa inakopesheka tena, lakini lazima
Wizara ya Fedha itumie uangalifu mkubwa katika kukopa ili Tanzania
ijikute inarudi tena katika mazingira yaliyopelekea kuachwa kukopeshwa
huko nyuma.



Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

15 Machi, 2011