Rais Jakaya Kikwete, ametangaza kuwa ataunda chombo maalum cha kupambana na ongezeko kubwa la tatizo kubwa la biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Aidha, Rais Kikwete amewaomba viongozi wa dini na taasisi za dini nchini kusaidiana na Serikali katika kupambana na tatizo hilo lenye madhara makubwa kwa jamii, na hasa miongoni mwa vijana ambao wanaunda asilimia 60 hadi 80 ya Watanzania wanaotumia dawa za kulevya ambazo zinaharibu mwili na akili ya mtumiaji.

Vile vile, Rais amesema kuwa wakati ni kweli kuwa mikoa yote ya Tanzania inakabiliwa na tatizo hilo, lakini ni mikoa saba inayoongoza kwa kuwa na tatizo kubwa zaidi ikiwa ni Dar es Salaam, Mwanza, Mjini Magharibi – Zanzibar, Arusha, Tanga, Mbeya na Dodoma.
Rais Kikwete alitangaza kusudio lake la kuunda chombo maalum cha kupambana na dawa za kulevya jana wakati wa sherehe za kusimikwa kwa Askofu Mteule Albert Jella Randa wa Kanisa la Mennonite, Tanzania, kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mwanza ambako alikuwa mgeni.
Sherehe hizo zilifanyika kwenye makao ya Dayosisi hiyo Nyakato, mjini Mwanza.
Akihutubia mamia ya waumini wa Kanisa hilo pamoja na wananchi wengine waliohudhuria sherehe hizo, Rais Kikwete amewaomba viongozi wa dini, madhehebu ya dini mbali mbali nchini kuongeza juhudi za kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Akisema kuwa pamoja na kwamba matunda ya juhudi za Serikali katika kupambana na tatizo hilo yameanza kuonekana bado kazi iliyoko mbele ya jamii ya Tanzania ni “kubwa sana”.
“Mwaka jana, 2010, watu 12,119 walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Katika kipindi hicho, dawa za kulevya zilizokamatwa ni heroine kilo 190 na gramu 780, cocaine kilo 65, morphine kilo 11, bangi kilo 279,520 na mirungi kilo 10,317. Takwimu zinaonyesha kuwa mkoani Mwanza tatizo linakua kwa kasi sana,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Dawa za kulevya zina madhara makubwa kwa watumiaji na kwa jamii. Kwa watumiaji hatima yake ni mtu kuharibikiwa kimwili na kiakili. Watu huwa mazezeta na hivyo kushindwa kutokuwa na manufaa kwa jamii. Hii ni hasara kwa familia, jamii na taifa. Bahati mbaya sana waathirika wengi ni vijana. Tafiti zilizopo zinaonyesha kwamba asilimia 60-80 ya watu wanaotumia dawa hizo ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 30, alisema.”
Aliongeza: “Hii ni hasara kubwa kwani vijana ndio nguvukazi ya leo na kesho. Ndiyo roho ya taifa na warithi wa familia, jamii na taifa. Wakiharibikiwa taifa letu litaangamia. Tusikubali. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kulichukia tatizo hili na kulikemea kwa nguvu zake zote ili kuokoa taifa letu. Nawaomba viongozi wa dini kushirikiana na Serikali na watu wote wenye mapenzi wa nchi yetu kupambana mpaka tufanikiwe kudhibiti na hatimaye kulitokomeza tatizo hili.”
Sherehe za leo za kusimikwa Askofu Randa (50) kuwa Askofu wa Kanisa Mennonite, Jimbo la Mwanza, pia zilihudhuriwa na mamia kwa mamia ya waumini wa Kanisa hilo na wananchi wengine.
Kwenye sherehe hizo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania (KMT), Mhashamu Severin Watson Mang’ana amemkabidhi askofu huyo mpya nguvu kuu ishara za mamlaka na madaraka ya uaskofu ikiwamo Biblia, Katiba ya KMT, Cheti cha Uaskofu na vitabu vya taratibu ya kuendesha ibada za Kanisa hilo na nyimbo.
Kanisa la Mennonite lililoanzishwa duniani mwaka 525 na Mchungaji Menno Simon mjini Zurich, Uswisi, liliingia nchini miaka 77 iliyopita mwaka 1934 na liko katika maeneo yote ya Tanzania isipokuwa Zanzibar, Ruvuma na Pwani. Kanisa hilo lina makao yake mkoani Mara.