Mwendesha mashtaka nchini Ivory Coast amesema kuwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Laurent Gbagbo, ameondoka kutoka mji wa Korhogo, kaskazini mwa nchi, na kwamba anasafirishwa hadi mahakama ya uhalifu wa kivita, mjini The Hague.

Taarifa iliyosomwa kupitia televisheni ya kitaifa iliyotiwa saini na mwendesha mashtaka huyo, imesema kuwa mahakama ya ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa bwana Gbagbo wiki iliyopita, ambayo alipokea hapo jana mbele ya mawakili wake.

Bwana Gbagbo amekuwa akizuiliwa katika mji wa Korhongo, Kaskazini mwa Ivory Coast, tangu mwezi Aprili.

Anatarajiwa kuwasili katika mahakama ya uhalifu wa kivita mjini The Hague, Uholanzi, leo asubuhi.

Maafisa wa mahakama wa Ivory Coast wamesema kuwa ndege iliyokuwa imembeba bwana Gbagbo tayari imeondoka kutoka uwanja wa ndege wa Abidjan na kuelekea Ulaya.


Serikali mpya ya sasa imekuwa makini kuona kwamba bwana Gbagbo ameondoka nchini humo kabla ya uchaguzi wa wabunge unaopangiwa kufanyika chini ya majuma mawili yajayo.

Kumekuwa na ripoti kuwa wafuasi wa Bwana Gbagbo waliojihami huenda wakavamia magereza na kuwaachilia wafungwa.

Bado sio wazi ni mashtaka yapi Bw Gbagbo atakumbana nayo mbele ya mahakama hiyo ya ICC, lakini takriban watu elfu tatu waliuawa katika machafuko ya baada ya uchaguzi , yaliyochochewa na uamuzi wa Bwana Gbagbo wa kubakia madarakani, hata baada ya uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba mwaka uliopita.