WACHEZA filamu ‘bei mbaya’ nchini, Wema Isaac Sepetu na Aunt Ezekiel Grayson (pichani) hivi karibuni nusura wazichape kavukavu kwa kisa cha kushangaza.

Ishu ilijiri juzikati katika Ufukwe wa Coco, jijini Dar es Salaam ambapo mastaa hao walikwenda kujirusha.
Chanzo chetu ambacho kilishuhudia ‘sinema’ nzima kilisema kuwa, Wema ndiye aliyetangulia kuwepo eneo hilo na ‘kampani’ yake, baadaye akawasili Aunt.

Chanzo kikazidi kuweka wazi kwamba, baadaye alitinga Wolper na kumsalimia Aunt kisha kila mmoja kuendelea na shughuli zake, lakini muda si mrefu, Aunt alijikuta akivutwa nguo kwa nyuma.

Kwa vile alikuwa hajajishika sehemu yoyote, yeye na aliyemshika walianguka chini kama zigo la mwizi.
Mpashaji wetu aliendelea kutupa mwendelezo wa sinema hiyo kuwa kipindi chote hicho Aunt hakujua ni nani, lakini alipobaini ni Wema alianza kumtania akijua hata kushikwa kwake ilikuwa katika hali ya utani.

Cha kushangaza, Wema alipoinuka alimrushia maneno Aunt akimuuliza ni kwa nini aliongea na Wolper wakati yeye ni adui yake.
“Walipoanguka chini Aunt alijua ni utani na kuanza kuongea na Wema kwa utani, lakini kumbe mwenzake alikuwa hayupo katika hali hiyo, alimrushia maneno makali kwamba kwa nini anaongea na Wolper wakati yeye ni adui yake,”kilisema chanzo.
Shuhuda huyo aliendelea kusema kuwa baada ya zogo hilo kuwa kubwa huku kila mmoja akipandwa na hasira, walitokea watu wenye busara zao na kuwaomba kila mmoja aondoke eneo lile ili kuepusha ugomvi zaidi.

Amani lilimuendea hewani Aunt na kumuuliza kuhusu ishu hiyo ambapo alikiri kutokea.
“Ni ishu ndogo tu ya kutoelewana, lakini mimi sipendi bifu hivyo mambo yaliisha pale pale,” alisema Aunt.
Wema yeye hakupatikana kwenye simu na habari zinasema yuko nje ya nchi.